Johnson ole Kiyaipi alizikwa kwa heshima kamili ya kijeshi nyumbani kwake Kenya baada ya kuuawa na bomu lililotegwa kando ya barabara nchini Somalia, ingawa jeshi wala serikali haijakiri hadharani kifo chake.
Mauaji ya kijana huyo wa miaka 35 na wenzake tisa wiki iliyopita, yanayodaiwa kutekelezwa na wanamgambo wa al-Shabab, yamechochea wito wa Kenya kuondoa wanajeshi wake kutoka Somalia, ambako wamekuwa wakipambana na kundi hilo la wanamgambo tangu mwaka 2011.
Ukimya huo rasmi umezidisha hali ya kufadhaika kwa familia ya Bw Kiyaipi huko Kilgoris, kusini-magharibi mwa Kenya.
"Tutawapoteza vijana wengine wangapi kabla vijana wetu warudishwe nyumbani? Bi familia zingine ngapi zitakabiliwa na machungu ya vita vinavyopiganwa katika nchi nyingine?" aliuliza kaka yake mkubwa, Dkt Joel ole Kiyiapi.
"kiwa vijana wetu watafariki, basi wafe wakilinda nchi yetu ndani ya mipaka yetu ."
Katika ibada ya mazishi , jeneza la Bw. Kiyapi lilibebwa juu ya mabega na wanajeshi wenzake na kupelekwa kwenye hema ndogo mbele yam amia ya wanavijiji waliohudhuria mazishi.
Jeneza lilikuwa limefunikwa bendera ya Kenya na juu yake kuwekwa kofia yake ya kijeshi mshipi na viatu.
Mkewe Bw Kiyaipi alitokwa na machozi wakati risala aliyokuwa amemwandikia mumewe iliposomwa na rafiki yake: "Mimi na watoto wako tutakukosa na tabasamu lako la kupendeza. Nuru iangaze njia yako mpenzi wangu," alisema katika hotuba hiyo.
"Umekuwa sehemu bora zaidi ya maisha yangu na kipenzi cha maisha yangu. Hujawahi kunitelekeza tangu niliposema: ''Nakubali kuwa mke wako," iliendelea kusema.
Mwili wa Bw Kiyaipi uliposhushwa kaburini, wanajeshi wenzake walimpatia heshima ya mizinga 21 huku baadhi ya waombolezaji waliokuwa wamezidiwa na huzuni wakianguka chini na kulia.
Kila mzungumzaji alisema familia nyingi zimepoteza wapendwa wao tangu Oparesheni Linda Nchi (Oparesheni ya Kulinda Nchi) ilipoanza miaka 11 iliyopita.
Hatua ya kijeshi iliyochochewa na tukio la kundi la wanamgambo kuwateka watalii wawili katika jimbo la Lamu karibu na mpaka wa Kenya-Somalia.
Miaka miwili baadaye, wanajeshi hao walijumuishwa katika Oparesheni ya Umoja wa Afrika nchini Somalia (Amisom), kikosi kilichoundwa kusaidia Somalia kuleta utulivu na kupambana na al-Shabab..
'Kwanini vifo vinafichwa?'
"Ikiwa Marekani ilijiondoa kutoka Somalia, sisi Wakenya nani tuendelea kukaa huko?" Mzee wa kijiji aliuliza.
"Tuna uchungu kwa kupoteza vijana Somalia. Wakati umewadia wa wao wa kurejea nyumbani na kulinda mipaka yetu," Joseph Tasur aliendelea.
Familia za wanajeshi hao zimekasirishwa na hatua ya serikali kusalia kimya wanajeshi wa Kenya wanapouawa vitani. Wanasema ukimya huo na kutokiri hadaharani mauaji hayo ni ishara ya kutowaheshimu. Mamlaka hazijaelezea kwanini zinasalia kimya kuhusu vifo vya wanajeshi.
Makadirio ya sasa yanaonyesha kuwa mamia ya wanajeshi wa Kenya wamekufa nchini Somalia, huku shambulio la El Adde la 2016 lililofanywa na wanamgambo wa Kijihadi lilisababisha vifo vya takriban 200.
Jeshi lilisema litafanya uchunguzi na kutoa maelezo ya wanajeshi waliofariki katika shambulizi hilo miaka sita iliyopita, lakini hadi sasa hili halijafanyika.
"Tunajua munailinda nchi yetu, munatulinda. Kwa nini tunawaficha askari wetu wanapokufa wakiwa kazini?" aliuliza Prof James ole Kiyaipi, ndugu mwingine wa Johnson, na mwanasiasa wa zamani.
'Serikali lazima iwe wazi'
Prof Kiyaipi alisema alishangazwa kuwa hakuna mjadala kati ya wabunge au umma kuhusu lengo la vikosi vya Kenya nchini Somalia.
"Tunahitaji kutafakari upya mkakati wetu na kuwa na tarehe ya mwisho iliyo wazi kwa wanajeshi wetu huko. Haiwezi kuwa oparesheniisiyo na kikomo na tuna hakika hatuwezi kumudu kuendelea kupoteza vijana wetu katika vita hivi," aliiambia BBC.
"Kila askari anayeuawa ni baba, mwana wa kiume au wa kike.Rais anahitaji kukiri hadharani vifo vya mashujaa wetu," aliendelea kusema.
"Sisi ndio walipakodi na serikali ina jukumu la kuwa wazi," alisema.
Kulikuwa na ghadhabu zaidi mtandaoni nchini Kenya wiki iliyopita wakati jeshi la Marekani lilipowatunuku wanajeshi watatu wa Kenya kwa ushujaa wao wakati wa shambulio la kambi ya Manda mnamo Januari 2020, huku serikali ya Kenya na vikosi vya jeshi vikisalia kimya kuhusiana na suala hilo.
Utambulisho rasmi pekee wa Wakenya ambao wameuawa wakiwa kazini ni makaburi ambayo yamezinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa siku ya kila mwaka ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya - utamaduni ulionzishwa baada ya jeshi kwenda Somalia.
Pia yana majina ya waliouawa wakipigana na al-Shabab, hivyo jina la Johnson ole Kiyaipi linatarajiwa kuongezwa.
Lakini, kambi hizi za kijeshi na makaburi ndani yake hayafunguliwi kwa umma.