Akiwa na kisu chenye ncha kali, kipaza sauti na akiwa amevalia mavazi meusi, Gbenga Adewoyin angeweza kuonekana kama mwindaji wa mchawi wa zama za kale, muuzaji mitishamba au mhubiri wa mjini alipokuwa akizunguka sokoni katika jiji la Ibadan kusini-magharibi mwa Nigeria.
Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo yanaweza kuwakera baadhi ya wasomaji
Wale waliokuwa na hamu ya kukaribia soko la Gbagi walitawanyika haraka waliposikia ujumbe wake. "Mtu yeyote ambaye anaweza kutoa ushahidi wowote wa kuwepo kwa miujiza, iwe juju au uchawi wa voodoo, atapewa naira 2.5m ($6,000, £4,650)," alitangaza mara kwa mara katika Kiyoruba na Kiingereza.
Mkana Mungu mwenye umri wa miaka 24 hivi majuzi ameibuka kama mwasi anayepinga hadharani uwezo wa miujiza katika nchi hii yenye imani kali za kidini .
Imani katika dini za kitamaduni za Kiafrika na vipengele vyake vya juju imeenea nchini Nigeria, huku wengi wakichanganya na Ukristo au Uislamu, kulingana na ripoti ya mwaka 2010 ya Kituo cha Utafiti cha Pew.
Wanigeria wengi wanaamini kwamba hirizi za uchawi zinaweza kuruhusu wanadamu kubadilika kuwa paka, kulinda ngozi tupu dhidi ya kukatwa na visu vikali na kufanya pesa kuonekana kwenye vyungu
Imani hizi hazishikiwi tu na wasio na elimu, zipo hata katika ngazi ya juu ya wasomi wa Nigeria.
Dk Olaleye Kayode, mhadhiri mkuu wa Dini za Asilia za Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Ibadan, aliiambia BBC kwamba mila ya juju ya kutengeneza pesa - ambapo sehemu za mwili wa binadamu vikichanganywa na hirizi hufanya pesa zitoke kwenye chungu - zinafanya kazi kweli.
Naira inaaminika kwamba inaonekana "iimechukuliwa na roho kutoka kwa benki zilizopo", aliiambia BBC.
Jude Akanbi, mhadhiri katika Seminari ya Theolojia ya Wahitimu wa Crowther huko Abẹ́òkúta, pia hana shaka kuhusu juju.
"Uwezo huu wa kuweza kujigeuza kuwa paka, kutoweka na kuonekana tena , mambo haya yanawezekana ndani ya mienendo ya dini ya jadi ya Kiafrika.
"Ingawa [inaonekana] kutokuwa na mantiki, kama hadithi za vikongwe, hata hivyo kutokana na kile tumeona na kusikia, mambo haya yanawezekana," alisema.
Imani hizo, hasa kwamba sehemu za mwili wa binadamu na hirizi zinaweza kutoa pesa kutoka kwa chungu cha udongo, zimesababisha wimbi la mauaji ya kutisha nchini hivi karibuni, huku wanawake wasio na waume mara nyingi wakiwa wahasiriwa.
"Ninajisikia vibaya kuona vijana wakijihusisha na mauaji haya ya kimila.
"Iwapo utaratibu wa pesa ulifanya kazi, tungeona mfumuko mkubwa wa bei katika uchumi kwa miongo kadhaa ambayo tumeamini," Bw Adewoyin aliambia BBC.
Alikuwa Ibadan, jimbo la Oyo, katika ziara ya pili kati ya tatu zilizopangwa za ndani ya nchi akitoa naira milioni 2.5, zinazofadhiliwa na watu kupitia Twitter, kwa yeyote anayeweza kuonyesha hadharani mamlaka haya ya juju.
"Kisu ni cha mtu yeyote anayedai juju yake inazuia makali kumchoma" alisema.
Kuhoji kuwepo kwa nguvu zisizo za kawaida kunachukuliwa kuwa mwiko katika sehemu kubwa ya jamii ya Nigeria.
Kueleza mawazo kama hayo kwa uwazi, kama Bw Adewoyin alivyokuwa akifanya sokoni, ilikuwa hatari. Angeweza tu kukamatwa kwa urahisi kwa kukufuru au kuuawa na kundi la watu wenye hasira.
"Kweli juju inafanya kazi, hajui anachosema," alisema mfanyabiashara mmoja ambaye alionekana kukerwa.
Mfukoni mwake kulikuwa na hirizi nyeusi, kipochi kidogo cha ngozi chenye eti hirizi za uchawi, ambacho alisema kilikuwa kwa ajili ya kumlinda . Hata hivyo, hakuwa na nia ya kuonyesha hadharani mamlaka yake, hata kwa $ 6,000.
Imani ya uchawi mara nyingi huambatana na Ukristo na Uislamu. Makasisi kutoka dini zote mbili za Mungu mmoja mara nyingi hurejelea vipengele vya dini za jadi za Kiafrika kama uovu - kitu halisi, lakini ambacho kinaweza kushindwa kwa maombi na nguvu zao za juu.
Wachungaji wengi wamekuwa matajiri na maarufu kwa madai ya kuwa na nguvu zisizo za kawaida ambazo zinaweza kushinda juju na laana mbaya, jambo ambalo maimamu wengi pia wanafanya.
Hata hivyo, hakuna aliyekubali changamoto ya Bw Adewoyin katika kumbi mbili za Ogun na Ibadan na hana matumaini ya matokeo tofauti katika kituo chake kingine katika jimbo la Anambra kusini-mashariki.
Ingawa amekataliwa na baadhi ya watu kama anayejivutia umaarufu , hakuna anayeweza kujificha kutokana na picha mbaya za miili iliyopatikana hivi majuzi ikiwa na viungo vilivyopotea na matundu ya macho katika kuzuka upya kwa mila mbovu ya kutengeneza pesa ya juju.
Mauaji haya ya wanadamu kutumia viungo vyao kwa ajili ya uchawi yaliikumba Nigeria katikati ya miaka ya 90 na kusababisha ghasia katika mji wa mashariki wa Owerri baada ya kutekwa nyara na kuuawa kwa mvulana wa miaka 11 mnamo 1996.
Sasa, kwa mitandao ya kijamii, ni vigumu siku kupita bila taarifa za mtu aliyepotea na picha za maiti zilizoharibika zilizohusishwa na juju.
Kulikuwa na ghadhabu kubwa mwezi uliopita baada ya wanaume watatu kudaiwa kumuua msichana mwenye umri wa miaka 17 katika jimbo la Ogun ili kutumia viungo vyake vya mwili katika tambiko ambalo waliamini lingewafanya kuwa matajiri. Walikiri kuhusika na mauaji hayo baada ya kukamatwa na polisi na kufunguliwa mashtaka mahakamani.
Chungu cha udongo na vitambaa vyekundu walivyonaswa navyo vingeweza kuchukuliwa kama tukio katika filamu kutoka Nollywood, tasnia ya filamu ya Nigeria maarufu kwa kuonyesha maonyesho ya juju, lakini hii ilikuwa kweli.
Na walikuwa vijana - mkubwa zaidi alikuwa na umri wa miaka 21, na hivyo kuibua hashtag ya Twitter #At21, ambapo watumiaji walielezea kile walichokuwa wakifanya katika hatua hiyo ya maisha na kuomboleza kile walichokiona kama shinikizo la jamii kwa vijana kupata utajiri wa haraka.
Hasira ya kifo cha msichana huyo ilifanya wabunge wa shirikisho kujadili juju bungeni na kuzingatia "tangazo la hali ya hatari juu ya mauaji ya kitamaduni nchini", na taswira yake katika sinema za Nollywood ikitajwa kuwa sababu.
Waziri wa Habari wa Nigeria Lai Mohammed pia amejitokeza, akilaumu sinema za Nigeria na mitandao ya kijamii kwa mfululizo wa mauaji.
Anataka bodi ya ukaguzi wa filamu kuwashirikisha watengenezaji filamu "juu ya haja ya kuepuka maudhui ya tambiko ya pesa katika filamu zao".
Lakini watengenezaji wa filamu wamekataa hilo - wanahisi anaionea Nollywood isivyostahili katika mzozo wa kitaifa.
"Waziri alikosea, hawezi kukiuka haki zetu za kimsingi za kuunda," mwigizaji na mtayarishaji Kanayo O Kanayo aliambia BBC.
Alisema waziri huyo anapuuza jambo ambalo limekuwa suala la jamii na kushindwa kwa familia, viongozi wa mila na dini na wanasiasa kuhakikisha vijana wanalelewa kimaadili .
Wakati mjadala ukiendelea kuhusu ni nani alaumiwe kwa mauaji hayo, mazungumzo mapana zaidi yanapaswa kufanywa kuhusu mfumo wa elimu wa Nigeria ambao unashindwa kuwashawishi watu kwamba juju na miujiza si ya kweli, anasema Bw Adewoyin.
Anatumai kwamba ziara yake ya uasi inaweza kuwafichua wale anaowaita wadanganyifu, wanaodai nguvu zisizo za kawaida za juju, na kusaidia kukomesha mfululizo wa mauaji ya kitamaduni.
"Kwa binadamu mwenye akili timamu kuamini kwamba binadamu akiwa na viambajengo vyake vyote vya kibaolojia anaweza kugeuka kuwa viazi vikuu au ndizi ni jambo lisilo na mantiki, na linatia wasiwasi," alisema.