Vita vya Ukraine: Urusi inaweza kutumia silaha za nyuklia ikiwa itakumbwa na tishio la kuangamizwa kabisa: Kremlin


 Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema katika mahojiano kwamba Urusi itatumia tu silaha za nyuklia ikiwa kuwepo kwake kutatishiwa.

Maoni ya Peskov yalikuja akihojiwa na kituo cha CNN na aliyasema wakati mtangazaji Christiane Amanpour alipomuuliza iwapo "ameshawishika au anajiamini" kwamba Rais Vladimir Putin hatatumia chaguo la nyuklia katika vita vya Ukraine .

"Tuna sera ya usalama wa ndani, na ni ya umma. Unaweza kusoma sababu zote za silaha za nyuklia kutumika," Peskov alisema Jumanne.

"Kwa hivyo ikiwa ni tishio linalowezekana kwa nchi yetu, basi inaweza kutumika kwa mujibu wa hali hiyo "

Putin mwezi uliopita aliamuru vikosi vya nyuklia vya Urusi kuwekwa katika hali ya tahadhari.

Sambamba na agizo hilo, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema mnamo Februari 28 kwamba vikosi vyake vya makombora ya nyuklia na meli za kaskazini na Pasifiki zimewekwa kwenye hali iliyoimarishwa ya mapigano, shirika la habari la Interfax liliripoti.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema mnamo Machi 14 kwamba "matarajio ya mzozo wa nyuklia, ambayo hapo awali haukuweza kufikiria, sasa yamerudi katika hali inayowezekana".

Peskov pia aliiambia CNN kwamba vita vya Urusi nchini Ukraine "vilikuwa vinaendelea kulingana na mipango na madhumuni ambayo yalianzishwa hapo awali".

Maoni hayo yanakuja baada ya Rais wa Marekani Joe Biden kuonya kwamba Putin anafikiria kutumia silaha za kemikali na kibaolojia nchini Ukraine, huku akieleza mbinu za Moscow kuwa za "ukatili".

Wiki iliyopita Urusi ilisema kuwa imerusha kombora lake la hypersonic la Kinzhal (Dagger) ambalo linaweza kulenga shabaha popote pale Duniani ndani ya saa moja.

Putin alisema mwezi Disemba kwamba Urusi ndiyo inayoongoza duniani katika makombora ya hypersonic, ambayo kasi yake inafanya kuwa vigumu kuidungua .

Makombora ya Kinzhal ni sehemu ya safu ya silaha iliyozinduliwa mnamo 2018. Urusi ilitumia kombora la hypersonic kwa mara ya kwanza wakati wa kampeni yake ya kijeshi nchini Syria mnamo 2016.

Vita hivyo vimetikisa makubaliano ya usalama wa ulimwengu baada ya Vita Baridi, kuhatarisha usambazaji wa mazao muhimu ulimwenguni, na kuibua wasiwasi kwamba kunaweza kuanzisha ajali ya nyuklia.

Kando, moto wa mwituni ulizuka karibu na kinu cha nyuklia cha Chernobyl kilichoacha kutumiwa Ukraine, lakini waziri wa maliasili wa nchi hiyo alisema kuwa miale hiyo imezimwa na mionzi ilikuwa ndani ya viwango vya kawaida. Chernobyl mnamo 1986 ilikuwa eneo la msiba mbaya zaidi wa nyuklia ulimwenguni.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post