Mzozo wa Ukraine: Mashambulio matatu ya Urusi mtandaoni yanayotia hofu nchi za Magharibi

 chanzo cha habari:bbc swahili

Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito kwa makampuni na mashirika ya kibinafsi nchini Marekani "kufunga milango yao ya kidijitali", akidai kuwa ripoti za kijasusi zinaashiria kwamba Urusi inapanga kushambulia Marekani mtandaoni.

Mamlaka za mtandao nchini Uingereza pia zinaunga mkono wito wa Ikulu ya White House wa "kuongeza tahadhari za usalama wa mtandao", ingawa hakuna hata mmoja aliyetoa ushahidi wowote kwamba Urusi inapanga shambulio la mtandao.

Urusi iliwahi kusema kuwa shutuma hizo ni za "Russophobic" -kuogopa Urusi.

Hahata hivyo, Urusi ni nchi yenye nguvu kubwa zana hatari mtandaoni, na wadukuzi wenye uwezo wa kfanya mashambulizi makubwa mtandaoni.

Ukraine haijatetereka na mashambulio ya Urusi mtandaoni lakini sasa wataalamu wanahofia Urusi huenda ikalipiza kisasi kwa kuwafanya mashambulizi ya kimtandao dhidi ya washirika wa Ukraine.

"Onyo la Biden linaonekana kuwa sawa, haswa wakati nchi za Magharibi zilipotangaza vikwazo zaidi, wanaharakati wa udukuzi wanaendelea kujiunga na vita, na masuala uvamizi huo yanaonekana kutopangwa," anasema Jen Ellis kutoka kampuni ya Rapid7 inayojishhughulisha na usalama wa kimtandao.

Hii ni udukuzi unaoogopwa zaidi na wataalamu.

BlackEnergy - ililenga kushambulia miundombinu muhimu

Ukraine mara nyingi huelezewa kama uwanja wa michezo wa udukuzi wa Urusi, ambayo imefanya mashambulio yanayoonekana kujaribu mbinu na zana.

Mwaka 2015 mkonga wa umeme wa Ukraine ulikatizwa na shambulio la mtandao linalofahamika kama BlackEnergy, ambalo lilisababisha kukatika kwa umeme kwa muda mfupi kwa wateja 80,000 wa kampuni ya huduma magharibi mwa Ukraine.

Ukrainian power station

CHANZO CHA PICHA,REUTERS

Maelezo ya picha,

Mkonga wa kitaifa wa umeme nchini Ukraine ulihambiliwa mara mbili na wadukuzi

Takriban mwaka mmoja baadaye shambulio lingine la mtandaoni lililojulikana kama Industroyer iliyokatiza umeme wa Kyiv, mji mkuu wa Ukraine, kwa karibu saa moja.

Marekani na Umoja wa Ulaya ziliwaelekezea kidole cha lawama wadukuzi wa kijeshi wa Urusi kwa mashambulizi hayo.

"Urusi inaweza kujaribu kutekeleza shambulio kama hili dhidi ya nchi za Magharibi kama kielelezo cha uwezo na kutoa taarifa," anasema mtaalamu wa masuala ya usalama wa mtandao wa Ukraine Marina Krotofil, ambaye alisaidia kuchunguza udukuzi huo wa kukata umeme.

"Hata hivyo, hakuna mashambulizi ya mtandao dhidi ya mkonga wa umeme ambayo yamesababisha kukatizwa kwa usambazaji wa umeme kwa muda mrefu. Kufanya mashambulizi ya mtandao kwenye mifumo changamano ya uhandisi kwa njia ya kuaminika ni vigumu sana na kufikia athari ya muda mrefu ya uharibifu wakati mwingine haiwezekani kutokana na ulinzi uliojengwa kutoka upande wa ndani."

Wataalamu kama Marina pia wanakisia kwamba hii inaweza kuleta madhara kwa Urusi pia, kwani nchi za Magharibi pia zina uwezo mkubwa na pia zina nafasi nzuri katika mitandao ya Urusi.

NotPetya Uharibifu usioweza kudhibitika

NotPetya inakisiwa kuwa ni shambulio la gharama kubwa zaidi la mtandaoni katika historia na mamlaka za Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya zinahusisha mashambulio hayo na kundi la wavamizi wa kijeshi wa Urusi.

Programu hiyo ya uharibifu ilifichwa katika programu ya software maarufu ya uhasibu inayotumiwa nchini Ukraine, lakini ilienea duniani kote kuharibu mifumo ya kompyuta ya maelfu ya makampuni na kusababisha uharibifu wa takriban dola bilioni 10.

Wadukuzi wa Korea Kaskazini walituhumiwa kusababisha ukatizaji mkubwa katika shambulio sawa na hilo mwezi mmoja kabla.

WannaCry

CHANZO CHA PICHA,WEBROOT

Maelezo ya picha,

WannaCry ransomware - hapa inaonyeshwa katika mazingira salama kwenye kompyuta ya mtafiti wa usalama

Kirusi cha Wannacry kiliharibu data katika takriban kompyuta 300,000 katika nchi 150. Huduma ya Kitaifa ya Afya ya Uingereza ililazimika kufuta idadi kubwa ya miadi ya matibabu.

"Aina hizi za mashambulizi zinaweza kusababisha fursa kubwa zaidi ya machafuko makubwa, kuyumba kwa uchumi, na hata kupoteza maisha," anasema Jen Ellis.

"Huenda isionekane kuwa na athari,lakini miundombinu muhimu mara nyingi hutegemea kuunganishwa kiteknolojia sawa na sehemu zingine za maisha yetu ya kisasa na tumeona uwezekano wa hilo kutokana na athari zakirusi cha WannaCry kwenye hospitali za Uingereza."

Hata hivyo, mwanasayansi wa kompyuta Prof Alan Woodward anasema mashambulizi kama hayo yana hatari kwa Urusi pia.

"Aina hizi za udukuzi zisizoweza kudhibitiwa zinafanana zaidi na vita vya kibaolojia kwa kuwa ni vigumu sana kulenga miundombinu muhimu katika maeneo mahususi. WannaCry na NotPetya pia zilikuw ana waathirika nchini Urusi pia."

Mashambulizi ya uhalifu mtandao yanazidi

Mnamo Mei 2021 Marekani ilitangaza hali ya hatari baada ya wadukuzi kusababisha bomba muhimu la mafuta kujifunga.

Customers queuing to fill up their cars on 11 May.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Maelezo ya picha,

Hofu ya kutokea kwa uhaba wa mafuta iliwafanya watu kununua petroli kwa wingi nchini Marekani

Bomba hilo la Kikoloni hubeba 45% ya usambazaji wa mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya ndege katika Pwani ya Mashariki na kukatizwa kwa usambazaji wake kulizua taharuki miongoni mwa Wamarekani..

Shambulio hili halikutekelezwa na wadukuzi wa serikali ya Urusi, bali na kikundi cha DarkSide kinachotumia kirusi cha kuteka, ambacho kinadhaniwa kuwa nchini Urusi.

Kampuni ya mafuta ilikiri kuwalipa wahalifu $4.4m (£3.1m) katika ugumu wa kufuatilia Bitcoin, ili kurejesha mifumo ya kompyuta.

BS,iliyoanzishwa nchini Brazil 1953,ni msambazaji mkubwa wa nyama duniani

CHANZO CHA PICHA,REUTERS

Maelezo ya picha,

JBS,iliyoanzishwa nchini Brazil 1953,ni msambazaji mkubwa wa nyama duniani

Wiki chache baadaye ugavi wa nyama uliathiriwa baada ya wadukuzi wengine wanaojulikana kama REvil kushambulia JBS, kampuni kubwa zaidi ya kusindika nyama ya ng'ombe duniani.

Moja ya hofu kubwa ya wataalam kuhusu uwezo wa mtandao wa Kirusi ni kwamba Kremlin inaweza kuagiza makundi ya uhalifu wa mtandao kuratibu mashambulizi dhidi ya malengo ya Marekani, ili kuongeza usumbufu.

"Faida ya kuagiza wahalifu wa mtandao kutekeleza mashambulizi ya ransomware ni machafuko ya jumla wanayoweza kusababisha. Kwa idadi kubwa ya kutosha wanaweza kusababisha uharibifu mkubwa wa kiuchumi," Prof Woodward anasema.

"Pia inakuja na bonasi iliyoongezwa ya kukanushwa kwa ukweli kwani vikundi hivi ni hatua iliyoondolewa kutoka kwa shambulio la serikali ya Urusi."

Je, Marekani ingejibu vipi?

Katika hali isiyokuwa ya kawaida endapo shambulio dhidi ya nchi mwanachama wa Nato itasababisha maafa au madhara ya data yasiyoweza kurekebishwa, basi Kifungu cha 5, kinachozungumzia ulinzi wa pamoja cha muungano huo kinaweza kutumika kujibu mashambulizi.

Lakini wataalam wanasema hii ingeweza kuiingiza Nato katika vita ambayo haitaki kuwa sehemu yake, kwa hivyo jibu lolote linawezekana kutoka kwa Amerika na washirika wa karibu.

Rais Biden tayari amesema kuwa "tuko tayari kujibu" ikiwa Urusi itaanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Marekani.

Hata hivyo, machafuko ya mtandaoni ambayo hayajawahi kushuhudiwa nchini Ukraine katika wiki za hivi karibuni kutoka kwa wadukuzi makini wa pande zote za vita yanaonyesha jinsi mambo yanavyoweza kuongezeka kwa urahisi. Kwa hivyo, hatua yoyote inaweza kuzingatiwa kwa uangalifu sana.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post