Martha Saipan ni mama wa mtoto mmoja , yeye ni Mkenya anayeishi na kufanya shughuli zake za kibiashara jijini Nairobi .
Akiwa na umri wa miaka 37 sasa anazungumzia maisha yake hasa katika ulimwengu wa kimapenzi kama sehemu ya maisha ambayo imempa machozi mengi sana . Kisa na maana ni kando na kupitia ndoa iliyojawa na vuta ni kuvute ukweli wa mambo haukosi kumjia kwamba mama yake mzazi na aliyekuwa mumewe wamekuwa na urafiki wa kimapenzi .
"Mimi na aliyekuwa mume wangu , tulikuwa hatujafunga ndoa rasmi ila tulianza kuishi pamoja kama wanandoa, siku zilivyosonga iliendelea kuwa vigumu kuwa katika ndoa kutokana na ugomvi na kichapo cha kila mara.Niliamua kutoka kwenye ndoa ile ila niligundua kwamba nilikuwa na ujauzito tayari "anakumbuka Martha.
Martha anasema kwamba ndoa yake na mumewe haikuwa ya miaka mingi waliishi pamoja kwa miaka miwili pekee , lakini ikawa somo kwake .
Mwanamke huyu anasema kwamba alichukua uamuzi wa kuanza kuishi na mama yake mzazi kutokana na ujauzito wake , baada ya kuacha maisha ya ndoa .
Mwaka wa 2007 alipojifungua mtoto aliaga dunia , kikawa kipindi chenye uchungu mwingi na sonona kwake , yeye aliendelea kuishi na mama yake hadi mwaka wa 2013 alipoamua kwamba aanze maisha yake mapya, kwa hiyo alipanga nyumba na pia kutafuta kazi ili kuendelea na maisha yake .
Ni hadi mwaka wa 2020 anasema kwamba alipokea simu ya dharura kutoka kwa mama yake akimsihi amuokoe kutoka kwa kipigo alichokuwa anakipata , alipofuatilia mama alimweleza ni kutoka kwa aliyekuwa mumewe.
"Niliandamana hadi nyumbani kwa mama na shangazi (dada mdogo wa mama) tulimkuta yule mwanaume wakiwa na mama , tulipomuuliza ni kwanini alikuwa anamshambulia mama alijibu , kwani kuna ubaya mume kumchapa mke wake ? Sote tulishangaa , ila mimi nilijipata katika butwaa zaidi nisijue la kufanya "anasema Martha
Ilikuwa ni siku ambayo mwanamke huyu anasema hatawahi kuisahau, kwani akiwa pale aligundua kwamba uhusiano wa mama na aliyekuwa mume wake ulikuwa umeanza zamani karibu miaka 15 , na kulingana na mwanadada huyu hicho ni kipindi walichokuwa wanaishi na aliyekuwa mumewe.
Ila anahoji ni vipi angemkabili mama yake mzazi na ukweli wote ulikuwa umejitokeza? Martha anasema kwamba imekuwa ni safari kuanza maisha ya kukubali kwamba mama mzazi alianza uhusiano na mtu aliyemtambua kama Mume na baba ya mtoto wake japo aliaga dunia akiwa mtoto mchanga , aidha anasema kwamba anapokumbuka siku za ndoa yake japo fupi, kila mara kulipokuwa na ugomvi kati yake na huyo mume wake mama alikuwa hafiki kusaidia kusuluhisha masaibu yao .
"Kila kitu kilianza kujiweka sehemu yake , taswira kamili ya uhusiano wangu na mama wakati wa ndoa yangu ilinijia, kwamba mama alikuwa hataki kuhusika na vita wala kesi za dhuluma nilizokuwa nimewasilisha katika kituo cha polisi dhidi ya vichapo vya kila mara kutoka kwa mume huyo'.Anakumbuka Martha
Mwanamke huyu anasema kwamba kutengana na mume wake mwaka 2006 kulisababishwa na mambo tofauti sana na hayakuwa na uhusiano wowote na alichokuja kugundua baadaye kati ya mama yake na mume wake wa zamani .
Anasema kwamba hakufikiria mama yake mzazi angemsaliti, ila anavyosema ni kuwa wote ni watu wazima ambao wamechagua kuwa wapenzi bila kufikiria gharama ya uhusiano wao kwake kama mtoto wa kipekee wa mama yake.
Uhusiano wake na mama umekuwa vipi tangu zamani ?
Alipozaliwa Martha Soipan , miaka ya themanini, alijikuta akiwa chini ya malezi ya mama wakiwa wanaishi na bibi .Ila ilibidi mama asafiri nje ya nchi kwa ajili ya ajira katika nchi za mashariki ya Kati , huku mwanadada huyu akiachwa chini ya malezi ya dada wa mama.
Wakati huo alikuwa na miaka miwili na alipotimu miaka 10 mama alirejea na kuchukua hatua ya kumuondoa mikononi mwa dada yake hadi shule ya bweni . Ni kipindi kilichokuwa na kiza kikuu kwani mwanadada huyu alikuwa mpweke hasa akiwa shule ya sekondari.
Mama alirejea kwa mara ya pili kutoka mashariki ya Kati kulingana na Martha , wakati yeye akiwa kama yatima na mara nyingi alijipata akiishi katika makao ya mwalimu mkuu hata baada ya shule kufungwa hasa akiwa sekondari. Hayo hayakumkatisha tamaa na ari ya kuwa na maisha mazuri baada ya kukamilisha masomo yake .
Japo anasema kwamba maisha yao yalikuwa ya kuhangaika na ilibidi mama na mwana wapige moyo konde kutafuta riziki.
Martha anasema kwamba licha ya matukio ya kwamba mama yake alianza kuwa na mahusiano na mtu aliyekuwa mume wake , aliwasamehe , ila uhusiano wao na ukaribu wao ulivunjika kabisa , na kwa sasa hawana mawasiliano yeyote .