Dini – nguvu nyuma ya rais mpya wa Kenya

 


William Ruto, ambaye anaapishwa kama rais mpya wa Kenya leo  Jumanne, ndiye rais wa kwanza wa kiinjilisti nchini humo na huenda akaweka dini katika mstari wa mbele  akiwa madarakani baada ya kutekeleza  jukumu muhimu katika ushindi wake wa uchaguzi.


Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 55 haoni haya kukiri hadharani imani yake na amekuwa akizungumzia masuala kama vile haki za mashoga na uavyaji mimba, ambayo huenda yakaibuka wakati wa uongozi wake.


Bw Ruto anapenda kunukuu maandiko, kusali na hata kulia hadharani. Wakati wa kampeni, wapinzani wake walimdhihaki kwa kumpa jina la  "naibu Yesu" – jina ambalo wafuasi wake walilikumbatia . 


Hatua yake ya kwanza baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha ushindi wake katika uchaguzi wa mwezi uliopita ilikuwa kupiga magoti na kusali pamoja na mkewe Rachel na viongozi wengine waliokuwa chumbani humo.


BwRuto na mkewe hata wamejenga kanisa katika makazi yao rasmi  mtaano  Karen katika jiji kuu la Nairobi.


Kiongozi wa Waislamu pia alisali katika boma hilo baada ya uamuzi huo, akionyesha kwamba licha ya imani kubwa ya Bw Ruto ya Kikristo, ana mpango wa kuwa kiongozi wa watu wa dini zote. Jamii  mbalimbali za kidini za Kenya kwa ujumla huishi pamoja kwa amani na rais mpya pia anafurahia kuungwa mkono na Waislamu wengi.


Askofu David Oginde wa Muungano wa Kiinjilisti wa Kenya alisema anatumai kuwa serikali ya Bw Ruto "itasimamia maadili na kuheshimu ukweli kwamba Kenya ni jamii ya kidini".


Kenya ni nchi ya waumini, huku hata Jaji Mkuu Martha Koome akihusisha uamuzi wa  Mahakama ya Juu iliyothibitisha ushindi wa Ruto kama "kazi ya Mungu" - badala ya mahakama yenyewe.


Akiwa naibu rais, ushawishi wake wa kidini kwa Rais anayemaliza muda wake Uhuru Kenyatta - Mkatoliki - pia ulidhihirika wakati wa muhula wao wa kwanza, haswa wakati wa harakati zao za kusafisha majina yao katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutokana na mashtaka yanayohusiana na ghasia zilizozuka baada ya mzozo mkali kuhusu uchaguzi wa 2007.


Wawili hao mara kwa mara walihudhuria makanisa ya kiinjilisti kusali, walipojaribu kuepuka kushtakiwa - jambo ambalo walifanikisha wakati upande wa mashtaka ulipoondoa mashtaka dhidi ya Bw Kenyatta mwaka wa 2014 na majaji wakatupilia mbali kesi dhidi ya Bw Ruto 2016.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post