Tarehe 2 Oktoba, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri. Siyo mabadiliko ya kwanza tangu aingie madarakani Machi 2021, na huenda yasiwe mabadiliko ya mwisho.
Haya ni mabadiliko ya tano madogo katika serikali ya sasa. Rais Samia alifanya mabadiliko ya kwanza mwezi Machi 2021, Ikulu Chamwino, Dodoma wakati wa hafla ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango.
Mabadiliko ya pili yalifanyika mwezi Septemba 2021. Mabadiliko ya tatu yalitangazwa Ikulu jijini Dar es Salaam, Januari, 2022. Mabadiliko ya nne, yalitangazwa kwa umma tareheKila wakati ambapo baraza la mawaziri linabadilika, kuna matokeo ya aina tatu hujitokeza. Mawaziri hubadilishwa kutoka wizara moja na kupelekwa wizara nyingine. Pili, mawaziri huondoshwa katika nafasi zao moja kwa moja. Tatu, mawaziri wapya huingizwa.
Katika mabadiliko haya ya sasa, Waziri Mpya ameingia katika Baraza, naye ni Angellah Jasmine Kairuki, akiteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Balozi Liberata Mulamula ameingia katika kundi la waliondoshwa barazani. Alikuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aliteuliwa katika nafasi hiyo wakati wa mabadiliko ya kwanza ya Machi 2021.
Innocent Lugha Bashungwa, na Dkt. Stergomena Lawrence Tax ni mawaziri walioingia katika kundi la kubadilishiwa wizara. Dkt. Tax akitoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kwenda Wizara ya Balozi Mulamula. Bashungwa katoka TAMISEMI na kwenda Wizara ya Ulinzi.
Historia ilioandikwa haijafutika
Dkt. Dkt. Stergomena Lawrence Tax aliandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi, nafasi ambayo haikuwahi kushikwa na mwanamke katika historia ya siasa za Tanzania tangu kupatikana uhuru.
Aliteuliwa wakati wa mabadiliko ya pili ya baraza la mawaziri yalipofanyika, Septemba 2021, kufuatia kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Tanzania. Awali alikuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Ameondoka katika Wizara hiyo na kwenda katika wizara nyingine kubwa na muhimu. Licha ya kwamba mwanaume ndiye amerudi katika Wizara ya Ulinzi; historia ya Dkt. Tax tayari imeshaandikwa na itabaki katika kumbukumbu.
Kwa hakika ni kazi ngumu kujua kipi kimechangia Balozi Mulamula kupoteza nafasi yake. Mwanadiplomasia na Mtumishi mwenye uzoefu wa kuzitumikia ofisi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za nje na ndani.
Ila ni kazi rahisi kujua kwamba mtu anayechukua nafasi yake, ambaye ni Dkt. Dkt. Stergomena Tax, ana uzoefu wa purukushani katika majukwaa kimataifa, baada ya kuhudumu SADC kutoka 2013 hadi 2021.
Uzoefu huo unamuweka katika nafasi nzuri ya kuweza kuitumikia Wizara hiyo kwa maslahi ya nchi. Na kwa upande mwingine, huduma ya Balozi Mulamula itaendelea kukumbukwa na kubaki katika historia.
Safari ya usawa wa Kijinsia
Septemba 15, 2021 akihutubia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Demokrasia, katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Rais Samia aliweka wazi mkakati wake wa kuendelea kuwateua wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi na kushughulikia haki za wanawake na usawa wa kijinsia.
Katika juhudi zake za kuwagusa wanawake, aliunda Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, ikiongozwa na Waziri, Dkt. Dorothy Gwajima. Wizara ambayo haijakumbwa na mabadiliko ya kiuongozi tangu Januari 2022.
Mabadiliko ya sasa hayajaongeza idadi ya Mawaziri wanawake. Kuondoka kwa Balozi Mulamula na kupandishwa Kairuki, mwanasiasa aliyepata kuhudumu wakati wa utawala wa Rais John Pombe Magufuli na Jakaya Kikwete, kumeifanya idadi ya mawaziri wa kike kubaki ileile tisa.
Mabadiliko madogo ya Januari 2022 ya baraza la mawaziri, ndiyo yaliyoongeza idadi ya mawaziri wa kike, kutoka saba na kufikia mawaziri tisa; katika baraza lenye takribani mawaziri ishirini na tano.
Licha ya kuwa idadi hiyo ni kubwa kulinganisha na mabaraza ya mawaziri yaliyopita katika serikali za nyuma. Mabadiliko ya hivi karibuni, yanadhihirisha kwamba malengo ya kuleta usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi yana safari ndefu.
Mambo manne muhimu
Mawaziri wateule katika Wizara tatu wamekula kiapo leo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Katika hotuba yake, Rais wa Samia amegusia mambo manne muhimu, ikiwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa mawaziri.
Mosi, ni kutumikia pande zote mbili za Muungano: “Katika viapo tunaapa kulinda, kuiheshimu na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano wenye pande mbili, na mtatumika sehemu zote sawa, kwa jinsi katiba ilivyogawa majukumu.”
Pili, Rais Samia amekumbusha juu ya utunzaji wa siri za serikali. Amewataka mawaziri wajue namna ya kuzisema na kuzifanyia kazi siri hizo. Tatu, kuelewa mipaka katika mamlaka ya utendaji.
La nne ni utii wa maelekezo ya serikali. “Linaloamuliwa na Serikali, wewe Waziri ni lako na unatakiwa ulibebe, ukalifanyie kazi kwa misingi uliyoelekezwa. Huwezi kusema nimeelekezwa hivi ila mimi nimetaka hivi.”
Katiba ya nchi inamruhusu kufanya mabadiliko wakati wowote na kwa idadi anayoitaka yeye. Kwa kulizingatia hilo, na bila ya kujali ni mara ngapi atafanya mabadiliko, sheria ya nchi inasimama upande wake. 31 Machi 2022 kutokea Ikulu ya Dodoma.