UNAAMBIWA kitendo cha Simba kudondosha pointi tatu jana kufuatia kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Azam kimeleta furaha Jangwani ambapo mabosi wa Yanga wametangaza vita kuwa sasa safari ya kutetea ubingwa imeanza rasmi na hawatafanya uzembe wowote wa kutumia mwanya huo kesho watakapoivaa Geita Gold.
Yanga itakuwa ugenini kesho kucheza na Geita Gold saa 10 jioni katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza huku ikiwa kileleni mwa ligi kwa pointi 17 wakati Simba ikikamata nafasi ya tatu kwa pointi 14.
Akizungumza leo Oktoba 28, 2022 jijini Mwanza katika mkutano na viongozi wa matawi ya timu hiyo Kanda ya Ziwa, Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said amesema kwa kuwa mtani wao amedondosha pointi wanapaswa kuitumia vyema fursa hiyo ambapo amewataka wanachama wa Yanga jijini hapa ni wenyeji kuhakikisha timu inapata ushindi na kukaa kileleni.
Amesema wanaheshimu mchango wa wanachama wao kwenye kila mkoa timu inapocheza hivyo wanawapa jukumu la kuhakikisha timu inapata ushindi na kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ilioubeba msimu uliopita.
“Tuhakikishe kesho tunakaa pale juu kwa tofauti ya pointi sita, biashara ni asubuhi na huu ni mwanzo tukusanye zetu mapema wameshaanza kuangusha bingwa anaanzia hapa kwenye hizi pointi tatu za kesho,”
“Tumekuja hapa kutafuta pointi tatu, hakuna kitakachotupa faraja kama pointi tatu na hizi alama tatu ziko mikononi mwenu (viongozi wa matawi, timu hii nimeikabidhi kwenu na sisi tutasikiliza maelekezo kutoka kwenu nyinyi ndiyo mnajua vitu gani vinahitajika ipate ushindi,”
“Hii siyo Yanga ya Injinia (Hersi Said) ni Yanga ya wana Yanga, tukija hapa tunakuwa wasikilizaji tunaomba ushindi wenu kuleta matokeo kwenye timu yetu,” amesema Injinia Hersi.
Mwenyekiti wa Yanga tawi la Mwanza Mjini, Salehe Akida aliitikia kwa kumhakikishia Rais Hersi Said kuwa asiwe na shaka na hilo kwani Mwanza haijawahi kuwaangusha. “Huwa hatufeli, uongo jamani? tumelipokea limekamilika,”.