BAADA ya kudumu kwenye soka la ushindani kwa takribani miaka 22 akicheza kwa mafanikio makubwa sana, Kipa Juma Kaseja ‘Tanzania One’ hatimaye amefanya maamuzi magumu kwa kutangaza kustaafu kucheza soka la ushindani mwaka huu.
Kaseja alianza kuonekana kwenye medani ya soka la ushindani mwaka 2000 akiichezea Moro United aliyojiunga nayo ikiwa Ligi Kuu akitokea Shule ya Sekondari ya Makongo na kucheza kwa msimu mmoja.
Mwaka uliofuata alijiunga na Simba aliyoicheza kwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 10 kwa misimu tofauti.
Pia, Kaseja aliichezea Yanga katika vipindi viwili kama ilivyo kwa Simba na baadaye alijiunga na Kagera Sugar kisha kutimkia Mbeya City na kumalizia KMC aliyoachana nayo msimu uliopita.
Kaseja pia katika kipindi hicho amekuwa akizidakia kwa nyakati tofauti timu za taifa kuanzia zile za vijana, wakubwa na hata ile ya ufukweni.
Staa huyo aliyesifika kwa kudaka umahiri wake wa kudaka akiwa na sifa ya kuokoa mara kwa mara mikwaju ya penalti mwanzoni mwa msimu huu alieleza ataendelea kudaka lakini kwa sasa ameeleza kupumzika.
“Bado ninaweza kucheza mechi za na kufanya vizuri lakini kwa sasa nimeamua kupumzika na kuwaachia wengine,” alisema Kaseja na kuongeza;
“Pamoja na kuacha kucheza mechi za kiushindani, nitakuwa kwenye familia ya soka na kufanya majukumu mengine pia nitakapohitaji nitacheza tu kwani bado nipo fiti.”
Kaseja ni kama aliandaa maisha yake baada ya kustaafu kuendelea kuwa kwenye soka kwani wakati akicheza alikuwa akisoma kozi za soka zilizotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na zile za CAF na sasa ni kocha wa Timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na ile ya vijana wasiozidi umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes. Pamoja na mengi Kaseja katika uchezaji wake, atakumbukwa kwa kuwa kipa aliyezifungia Simba na Yanga.
Tags
michezo