ECOWAS yapitisha utaratibu wa sarafu moja



Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi - ECOWAS imepitisha utaratibu mpya wa kuzindua sarafu moja ifikapo mwaka 2027 baada ya mipango yake ya awali kukatizwa na janga la virusi vya corona. Akiwahutubia wanahabari baada ya mkutano wa viongozi wa mataifa ya jumuiya hiyo nchini Ghana jana Jumamosi, Jean-Claude Kassi Brou, rais wa halmashauri kuu ya jumuiya hiyo amesema kuwa utaratibu huo ulikubaliwa na viongozi hao. Brou amesema, kutokana na janga la virusi vya corona, viongozi hao waliamua kuahirisha utekelezaji wa mkataba huo wa pamoja katika kipindi cha mwaka 2020-2021. Mataifa hayo yanaamini kuwa sarafu moja itasaidia kuimarisha biashara na ukuaji wa uchumi. Nigeria, taifa lenye uchumi mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Magharibi, kwa sasa inatumia sarafu yake binafsi ya naira huku mataifa manane mengine, ikiwemo Ivory Coast yakitumia sarafu moja ya CFA inayoungwa mkono na Ufaransa, thamani yake ikifungamanishwa na Euro.



Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post