Rais Samia apangua wakuu wa wilaya

 



Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa wakuu wa wilaya nchini ambapo amewabadilisha vituo vya kazi baadhi, ameingiza sura mpya na kuwarudisha waliowahi kushika nafasi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Juni 19,  2021  na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Jaffar Haniu, Rais Samia ameteua watu wa kada tofauti wengi wakiwa  vijana.

Katika orodha hiyo, Rais Samia amewateua waandishi wa habari kushika nafasi hiyo. Walioteuliwa ni Fatma Almas Nyangasa wa Azam TV (Kigamboni), Simon Simalenga wa Clouds Media Group (Songwe) na Abdallah Mwaipaya wa ITV/Radio One (Mwanga).

Vilevile, Rais Samia amewateua baadhi ya waliokuwa wabunge lakini kwa sababu mbalimbali wakashindwa kurejea bungeni. Wateule hao ni Joshua Nassari (Bunda), Halima Bulembo (Muheza) na Peter Lijualikali (Nkasi).

Rais Samia amewateua pia waliokuwa viongozi wa upinzani wakahamia CCM. Wateule hao ni pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji (Serengeti), aliyekuwa meya wa Arusha, Kalist Lazaro (Lushoto), aliyekuwa mwanasheria wa ACT Wazalendo, Albert Msando (Morogoro).

Rais amemrudisha pia Sophia Mjema katika nafasi ya mkuu wa wilaya na sasa ataongoza wilaya ya Arusha. Mjema ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Ilala alipoteza nafasi hiyo baada ya kutangaza nia ya kugombea ubunge mwaka jana.

Baadhi ya wakuu wa wilaya waliohamishwa vituo vya kazi ni pamoja na Godwin Gondwe (Kinondoni), Jokate Mwegelo (Temeke), Sarah Msafiri (Kibaha) na Jerry Muro (Ikungi).

Baadhi ya waliotoswa katika uteuzi huo ni pamoja na Lengai Ole Sabaya ambaye alikuwa mkuu wa wilaya ya Hai kabla ya kusimamishwa kwa tuhuma mbalimbali na Simon Odunga ambaye alikuwa mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara.

"Wakuu wa wilaya wateule wataanza kuapishwa kuanzia Juni 21 saa 4 asubuhi na wakuu wa mikoa yao," inaeleza taarifa hiyo ya Ikulu.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post