Wahandisi wa maji 188 waliozingua watemwa na Serikali

 


Mwanza. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wizara hiyo imeachana na wahandisi wa maji 188 ikiwa ni hatua ya kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi.

Akizungumza leo Jumatatu Juni 14, 2021 kwenye hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji na usafi wa mazingira wa mji wa Misungwi, Aweso amesema wizara hiyo haiwezi kufanya kazi na wahandisi wababaishaji.

“Kampuni ya makandarasi 69 tushaachana nayo ili kujipa ushindi na kuhakikisha tunamtua mama ndoo kichwani, wahandisi wababaishaji hawana nafasi katika wilaya hii  na tushafanya tathmini na watendaji wangu..., mkeka mwingine unatoka hivi karibuni kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kuweza kupata maji safi na salama,” amesema Aweso.

Kuhusu miradi isiyo na ubora aliyoiita miradi kichefuchefu, Aweso amesema wameainisha miradi hiyo 177 ambayo licha ya kukamilika lakini haitoi maji na kati ya miradi hiyo, 85 wameikwamua na inatoa maji.

Aweso amesema wizara yake haipo tayari kuzinguana na Rais Samia na kuwataka watendaji wake kutokuwa kikwazo cha Watanzania kupata maji safi na salama.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post