Dubai inapitia kipindi kigumu cha hali mbaya joto kali. Eneo hilo ndani ya Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE) lina joto kali linalovuka mpaka nyuzijoto 50 na kuhatarisha maisha ya watu zaidi ya milioni 3 wanaoishi katika mji huo.
Hivi karibuni nchini Canada zaidi ya watu 500 waliripotiwa kufariki dunia kwa sababu ya joto kali. Kuepuka madhara hayo UAE kupitia kitengo cha hali ya hewa kimekuja na teknolojia inayoweza kupunguza hali hiyo ya joto, na teknolojia hiyo ni utengenezaji wa mvua feki.
Kituo cha hali ya hewa cha nchi hiyo kupitia tovuti yake, wiki hii kilichapisha video kupitia mtandao wake wa twitter ikionyesha mvua hiyo kubwa kiasi iliyokuwa inanyesha kwenye maeneo kadhaa huku watu wakiendelea na maisha yao ya kawaida na magari yakionekana yakipita kwenye barabara kubwa zenye mvua.
Mwisho wa Twitter ujumbe, 1
Zilitumwa ndege zisizo na rubani kwenye mawingu yaliyo usawa wa kando kidogo ya mji wa Dubai ili kutekeleza teknojia hiyo, ambayo imeanza sasa kufanyiwa majaribio .
Teknolojia hiyo inafanyaje kazi?
Kwa mujibu wa taarifa za kitengo cha hali ya hewa cha UAE ni kwamba, zimetengenezwa ndege ndogo maalumu zisizo na rubani (Drones), ambazo zimewekewa nguvu maalumu ya umeme.
Ndege hizi zinatumwa angani kwenye mawingu zikifika huko zinaruhusu umeme ambao huleta mshituko ama kupiga shoti mawingu na kuyasukuma mawingu hayo kubadili muundo wake.
Kubadilika huko kunasababisha unyevu nyevu na maji maji ambayo yakidondoka ardhini yanakuwa mvua ambayo haina tofauti yoyote na mvua iliyozoeleka.
Mtaalam mbobezi anayefanya kazi kwenye mradi huo wa mvua feki Prof Maarten Ambaum, aliwahi kunukuliwa na BBC kuhusu mradi huo na miradi mingine ya mvua feki hasa wakati huu nchi hiyo ikikumbwa na joto akisema 'nchi hii ina mawingu mengi sana, kwa hiyo mpango uliopo ni kusukuma mawingu haya ya matone ya maji yaweze kushikamana kama nywele kavu wakati yatakapokutana na umeme',
"Matone haya yakiungana na kuwa makubwa, yanadondoka, yanapodondoka yanakuwa mvua."Alisema.
Alya Al-Mazroui, Mkurugenzi wa Kitengo cha masuala ya utafiti wa mpango wa mvua za ziada alisema wakati wa majaribio ya mpango ama teknolojia hii "hizi ndege zitapaa kwenye anga la chini na kurusha umeme huo kwenye mawingu na kuleta mvua."
Ni rahisi kutengeneza mvua feki?
Kwa watafiti wanaeleza maoni tofauti kwenye teknolojia hii ya mvua feki, lakini wengi wanakubaliana kwamba ni gharama kubwa kufikia malengo ya mvua inayohitajika kwenye nchi ama eneo fulani.
Katika Falme za Kiarabu, serikali imeipa kipaumbele miradi ya aina hii na imekuwa ikitenga fedha kusaidia utekelezaji wake.
Nchi hiyo tayari inatumia teknolojia nyingine ya kumwagia mawingu chumvi. Ndege zisizo na rubani hurushwa angani na kwenda kudondosha chumvi kwenye mawingu na kusababisha mvua. Ndege hizi za aina hii zinapaswa kuwa nyingi kutekeleza azma iliyokusudiwa hivyo kuzidi kuongeza gharama.
Mwaka 2017, Serikali ya UAE ilitoa kiasi cha dola $15m kwa ajili ya miradi 9 ya kusaidia kutengenezwa kwa mvua feki. Wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Reading ni miongoni mwa wataalamu wanaoendesha moja ya miradi hii.
Mvua feki ni salama kwa Dubai?
UAE hasa eneo la Dubai hupata mvua chache sana kwa mwaka, kiasi cha 100mm pekee ambacho ni kidogo mno, kutokana na mazingira na hali yake ya ukame. Kwa hilo joto kuongezeka huwa ni jambo la kawaida nchini humo, kiasi cha kuufanya hasa mji wa Dubai, ambao unatajwa kuwa miongoni mwa miji ya kitalii inayopendwa duniani kuwa na joto jingi kupindukia . Kwa sasa Mamlaka za hali ya hewa zinapambana kuongeza kiwango zaidi cha mvua ili kupunguza joto.
UAE imekuja na mpango huo wa Mvua feki ambao umeanza kufanyiwa majaribio Dubai, lakini maswali mengi yanaibuka kuhusu usalama wake. Je mradi huo hauwezi kusababisha mvua kubwa za maafa?
Kwa nmna ilivyoonekana, majaribio ya mradi huu wa mvua feki yameenda vizuri na kufanikiwa. Kulikuwa na vitaa vidogo vidogo vya njano vingi angani vilivyotoka kwenye ndege ndogo zisizo na rubani kuashiria kwamba, ndege hizo zimefanikiwa kutekeleza kilichokusudiwa. Ndege yoyote iliyotumwa kwenye mawingu ingewasha taa nyekundu ama chochote tofauti na taa ya njano, maana yake imeshindwa kufikia lengo.
Lakini wakati wa majaribio kuna wakati mvua hizo zilikuwa kubwa zaidi na kuibua maswali mengi kuhusu hasara za mradi huo wa mvua feki. Bado maswali yanabaki kuhusu usalama wake na namna ya kudhibiti iwapo mvua hizo zitaongezeka na kuwa kubwa zaidi kutokana na umeme wa ndege hizo zinazotumwa kupiga mawingu.
Mpango huu wa UAE hasa Dubai wa kutengeneza mvua feki unaandaliwa kuwa mpango mkubwa zaidi na utakaoweza kutumia ndege kubwa zaidi badala ya ndogo zisizo na rubani, ili kuufanya kuwa mradi kabambe katika siku za usoni.