Hospitali ya KCMC yazidiwa na idadi ya wagonjwa wanaohitaji Oksijeni


Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini, KCMC imezidiwa na idadi ya wagonjwa wanaohitaji hewa ya Oksijeni ukilinganisha na mitungi 400 inayozalishwa kwa siku huku mgonjwa mmoja akitumia mitungi 8 hadi 10 kwa siku.

Hayo yamesemwa leo Ijumaa Julai 23 na Mkurugenzi Mtendaji Hospitali hiyo, Profesa Gilleard Masenga wakati akizungumza na Mwananchi Digital.

Profesa Masenga amesema kwa siku inatumika mitungi ya Oksijeni zaidi 400 ukilinganisha na uzalishaji wake kwa siku ambayo ina uwezo wa kuzalisha mitungi 400.

"Kwa siku mgonjwa mmoja anatumia mitungi 8 hadi 10 hili tatizo ni kubwa na wananchi msilichukulie kimzaha mzaha ni ugonjwa hatari sana, tuendelee kuchukua tahadhari zote zinazotolewa na Wizara ya Afya," amesema Profesa Masenga na kuongeza,

"Tuna kiwanda hapa KCMC cha kuzalisha mitungi 400 kwa saa 24 na mtambo huu Mungu alitusaidia tukauweka mwaka jana na tuliona hili litatusaidia kwa miaka 20 bila kuwa na shida ya Oksijeni,"

"Matumizi yetu kwa siku yalikuwa ni mitungi 50 hadi 60 lakini ilipofika mwezi wa tatu mwaka jana kwenye wimbi la kwanza la corona tuliona umuhimu wake,"Mwananchi Digital ilimnukuu Profesa Masenga.

Katika hatua nyingine hapo jana, serikali ya Tanzania imepiga marufuku shughuli zote za misongamano yote isiyo ya lazima, ikionesha kutorodhishwa na hali ilivyo katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo katika kuchukua hatua za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.

Wizara ya Afya imesema Hali hii imeendelea kuchangia kuongezeka kwa maambukizi na kufanya idadi ya wagonjwa waliolazwa kuongezeka ambapo kufikia tarehe 21 Julai katika vituo vyote vya afya nchini humo kulikuwa na wagonjwa 682 waliokuwa wakiugua Covid-19.

Halikadhalika serikali ya Tanzania imetoa wito kwa raia kujiandaa kupata huduma ya chanjo.

Taarifa ya Wizara ya afya imesema wataalamu wa afya wamekutana kupata mafunzo tayari kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma ya chanjo dhidi ya Covid-19.

Virusi vya Corona: Serikali ya Tanzania yaonya kuhusu wimbi la tatu la Corona

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post