Julai 18 kila mwaka dunia huadhimisha siku ya kimataifa ya Nelson Mandela, rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya Kusini huru. Maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika wakati nchi hiyo ikiwa katika maumivu ya ghasia za zaidi ya juma moja.
Machafuko ya hivi karibuni nchini Afrika Kusini yamesababisha mshtuko barani Afrika na nje ya bara hilo. Machafuko hayo yalizuka baada ya rais mstaafu Jacob Zuma kujisalimisha, akitii amri ya mahakama iliomhukumu kwenda jela miezi 15.
Kisa ni kupuza kuhudhuria kufika mahakamani mara kadhaa kama alivyotakiwa, katika uchunguzi unaohusiana na mashtaka ya rushwa yanayomkabili.
Uharibifu wa mali katika machafuko hayo ulikuwa usio na kifani, sio tu maduka ya bidhaa muhimu yalioporwa na kuchomwa moto lakini pia majengo ya maduka makubwa ya biashara,viwanda mbali na kuharibiwa miundo mbinu, zikiwemo barabara na vibanda vya mawasiliano ya simu mitaani.
Matukio haya yamekuja katika wakati kukiripotiwa wimbi kubwa la maambukizi ya Covid-19. Baadhi ya wakaazi walilazimika kuunda vikundi kulinda na kuzinusuru mali zao.
Sehemu kubwa ya machafuko ilikuwa katika Mkoa wa Kwazulu Natal, anakotoka Zuma na Gauteng kuliko mji mkuu wa kiuchumi wa Johannesburg.Gauteng pia ndiko uliko mji wa Pretoria,makao makuu ya kisiasa.
Chanzo cha machafuko
Machafuko hayo yalianza kama maandamano ya malalamiko dhidi ya kuwekwa jela rais wa zamani Zuma, baada ya kujisalimisha. Zuma alihukumiwa na mahakama kuu kifungo cha miezi 15 kwa kudharau mara kadhaa amri ya kumtaka afike mahakamani katika uchunguzi unaohusina na kesi ya rushwa inayomkabili.
Maandamano yaligeuka sio tena ya kudai Zuma aachiwe huru, lakini kilio cha wananchi wa kawaida,wale wanaoitwa walala hoi na wanyonge, juu ya hali ngumu za maisha. Wakosoaji wanasema kisa cha Zuma kilikuwa sababu tu.
Afrika Kusini ina kiwango kikubwa cha uhalifu na changamoto kubwa inazokabiliana nazo leo ni ukosefu wa usawa katika jamii, idadi kubwa ya wasio na ajira na huduma mbaya kwa umma, jambo ambalo linawaathiri zaidi waafrika kusini weusi.
Ukosefu wa ajira unawakumba zaidi vijana, wakiwemo wanaomaliza vyuo vikuu kila mwaka wakiwa hawana matumaini kuhusu mustakbali wao na kujikuta sawa na wasiomaliza shule.
Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia, asilimia 37 ya vijana wa Afrika Kusini hawana kazi na ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa duniani.
Wanyonge na ahadi za ANC
Lawama zinaelekezwa kwa chama tawala African National Congress-ANC, chama kikongwe kabisa barani Afrika kilichoundwa 1912,kwa kushindwa kutimiza ahadi zake kwa waafrika weusi.
Chama hicho cha mshindi wa kwanza wa tuzo ya amani ya Nobeli Chifu Albert Lithuli 1960, kiliahidi kuwapatia elimu, huduma ya afya, makazi bora na maji safi, baada ya kushika madaraka ya kuliongoza taifa hilo, kufuatia kumalizika sera ya ubaguzi wa rangi ya wazungu wachache Apartheid.
Miaka 27 tangu ulipofanyika uchaguzi wa kidemokrasi Aprili 1994, serikali ya ANC imeshindwa kutekeleza angalau sehemu ya ahadi hizo za tangu enzi ya mapambano ya ukombozi ili kuwa na Afrika Kusini yenye usawa kwa watu wa rangi zote.
Utwaaji ngwira madukani ulionekana kufanywa pia na waafrika kusini wa jamii nyengine wakiwemo wazungu, tukio ambalo limebainisha kwamba si Weusi peke yao wenye kuishi katika mazingira magumu ya kimaisha lakini pia wenye asili ya kizungu na kihindi na machotara.
Kwa maneno mengine janga hilo ni la raia wa taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa madini kwa jumla.
Katika hotuba yake kwa taifa Ramaphosa alionya kwamba serikali yake haitovumilia kuona nchi haitawaliki na akasema uchunguzi umebaini kulikuwa na kundi la watu 12 waliopanga makusudi fujo hizo, akiuita mpango huo kuwa shambulio dhidi ya demokrasia.
Pamoja na serikali kuwatawanya wanajeshi 25,000 katika maeneo ya ghasia kurejesha utulivu Ramaphosa aliondoa uwezekano wa kutangaza hali ya hatari.
Kujitajirisha viongozi wa ngazi ya juu
Viongozi wa ngazi ya juu wa ANC katika serikali na chama wanashutumiwa kwa kujitajirisha na kutumbukia katika ufisadi na rushwa. Katika hilo wanaelekezewa kidole kuwa matajiri wakubwa ni pamoja na Rais Ramaphosa ambaye ni bilionea na aliyekuwa Waziri mkuu wa kwanza wa mkoa wa Gauteng Tokyo Sekwale.
Ramaphosa ni kiongozi wa zamani wa Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (COSATU) wakati wa utawala wa kibaguzi,ambaye sasa anatajwa kuwa mmoja wa wenye hisa katika kampuni ya madini ya Lonmin.
Katika hilo la utajiri Zuma - mwanasiasa ambaye ni maarufu miongoni mwa maveterani wa vita vya ukombozi wa jeshi la wapiganaji wa ANC-Umkhonto Wesizwe (Mkuki wa Taifa) na miongoni mwa waliokuwa jela pamoja na Nelson Mandela katika gereza la Roben, hakunusurika. Mwaka 2005 alihusishwa na kashfa ya zabuni ya ununuzi wa silaha kutoka Ulaya kwa ajili ya jeshi la Afrika kusini, wakati huo akiwa Makamu wa Rais Thabo Mbeki, pamoja na mshauri wake wa fedha Schabir Shaik. Shaik alihukumiwa miaka 15 jela.
Kashfa hiyo iliuweka wazi ule mvutano wa Zuma na Mbeki. Zuma aliondolewa Umakamu wa Rais lakini akabaki kuwa Naibu Rais wa ANC.Sheikh alihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela.
Mbeki aliamua kumzuwia makamu wake wa Rais asiwe mrithi wake pale atakapomaliza muda wake.
Lakini Zuma aliyekuwa na ufuasi mkubwa ndani ya ANC, aliwekewa kifua na wanachama waliomuunga mkono. Uchunguzi ulipobaini Mbeki alitumia vyombo vya dola katika njama ya kutaka kumzuwia, mkutano mkuu wa chama akalazimika ajiuzulu ikibakia miezi 8 tu na kipindi chake cha pili na cha mwisho kumalizika. Zuma alipitishwa kuwa mgombea na akashinda Urais 2009.
2018 kibao na yeye kikamgeukia alipolazimika na yeye kujiuzulu kutokana na kashfa ya familia Tajiri ya Gupta. Familia hiyo ilitajwa kuwa na ushawishi mkubwa wa maamuzi ya Zuma.
Kuna ile kashfa nyengine ya matumizi ya mamilioni ya fedha za serikali kukarabati makazi yake kijijini kwao, Kashfa iliozusha kelele bungeni kutoka chama cha Economic Freedom Fighter-EFF. Wabunge wa EFF kilichoanzishwa na Julius Malema, kiongozi wa zamani wa chama cha vijana wa ANC, walizivuruga shughuli za bunge mara kadhaa kwa kelele za " Zuma must go" (Zuma lazima aondoke).
Zuma anakabiliwa na mashtaka 16 ya rushwa, udanganyifu, kutolipa kodi na utakasishaji fedha. Binafsi anasema anaandamwa na maadui zake ndani ya ANC.Wadadisi wanaashiria machafuko ya karibu na kesi ya ufisadi, huenda ni kuukomelea msumari wa mwisho katika shughuli za kisiasa za Zuma.
ANC na mtihani unaoikabili
Wakati huo huo ANC inakabiliwa na mtihani mkubwa. Ingawa kinaendelea kuungwa mkono na wengi, lakini imani kwa chama hicho inazidi kupunguwa, huku kikionekana kupoteza dira na kuwaacha wanyonge, shina la umaarufu wake, bila ya matumaini juu ya mustakbali wao.
Hali iliyoikumba ANC pamoja na ubaya wake kwa jumla lakini inaweza kutizamwa kama kipimo cha kukabiliana na changamoto inazokabiliana nazo jamii, kabla ya uchaguzi mkuu 2024.
Machafuko yamegeuka njia ya wenye hali duni za maisha kuonesha hasira zao. Wanahisi ile kauli mbiu ya "Amandla " (Madaraka ) kwa Umma, bado haikuwaletea mafanikio waliyoyatarajia.
Hii si mara ya kwanza kunatokea machafuko na mashambulio dhidi ya maduka na uporaji mali Afrika Afrika.
2008 na 2009, waliandamwa wahamiaji walioshambuliwa na mali zao kuchomwa moto. Miongoni mwao ni kutoka Somalia na Zimbabwe. Washambuliaji walidai wahamiaji hao wanachukuwa nafasi zao za kazi.
Nje ya mipaka yake, ile sura ya Afrika Kusini kuwa taifa la kusimamia amani kwenye maeneo ya migogoro barani Afrika, sasa inaekewa alama ya kuuliza,kwasababu ya ukosefu wa amani na utulivu ndani, kwake yenyewe.