Makundi ya haki yaituhumu Iran kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji
Makundi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanasema Iran inatumia nguvu kupita kiasi katika mapambano na waandamanaji wanaolalamikia uhaba wa maji katika mkoa wa kusini magharibi wa Khuzestan. Shirika la Amnesty International lililo na makao yake makuu mjini London linasema limethibitisha kuwa karibu waandamanaji wanane akiwemo mvulana mmoja wamefariki dunia baada ya polisi kutumia risasi za moto kutuliza maandamano. Vyombo vya habari vya Iran kwa upande wake vimesema watu watatu ndio waliofariki dunia akiwemo afisa wa polisi na mwandamanaji. Shirika la Human Rights Watch nalo katika taarifa yake linasema uongozi wa Iran ulionekana kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na limeitaka serikali ichunguze vifo hivyo vilivyoripotiwa.