Sir Richard Branson ametaja tarehe ambayo atafanya safari ya anga za juu.
Safari hiyo itakuwa Julai 11, au siku za karibuni baada ya tarehe hiyo.
Atakuwa abiria wa nyuma katika roketi ambayo kampuni yake ya Virgin Galactic iliitengeneza nchini Marekani kwa karibu miongo miwili.
Chombo hicho kinaweza kuruka katika urefu wa kilomita 90 (futi 295,000), na kuweza kuwapa fursa abiria waliopanda kuweza kuangalia mandhari ya dunia kutoka juu kwa dakika chache.
Nia ya Sir Richard ni kuanzisha biashara ya huduma ya safari za anga.
Watu wapatao 600 tayari wamelipia ili waweze kusafiri katika mpango huo.
Kumshuhudia mjasiriamali wa Uingereza akipanda roketi hiyo ina maanisha kuwa wateja wanakaribia kukabidhiwa tiketi na zitagharimu dola $250,000 (£180,000).
Sir Richard Branson alisema: "Kiukweli ninaamini anga ni yetu sote. Baada ya miaka 17 ya utafiti, uhandisi na ubunifu wa sekta mpya ya biashara ya anga ninaamini kuwa itafungua fursa nzuri ya mabadiliko katika dunia.
"Ni jambo moja kuwa na ndoto ya kuifanya anga iweze kufikika na kila mmoja, na ni suala jingine kwa kikosi cha kushangaza kuifanya ndoto kuwa uhalisia."
Kiukweli nguzo ya kampuni ya Virgin Galactic kuendeleza biashara zake ni kupata leseni ya biashara ya anga kutoka kwa mamlaka ya anga wiki iliyopita.
Jumapili ya Julai 11, itazindua kile walichokiita maonesho ya ndege.
Kikosi cha Galactic kinalenga kupaa siku hiyo lakini kunaweza kuwa na sababu ya kucheleweshwa kwa safari yao kutokana na hali ya hewa au hitilafu za kiufundi.
Wally Funk atakuwa mtu wa umri wa juu zaidi kwenfa anga za juu akisafiri na Jeff Bezos
Kama mpango wao utaendelea Jumapili, itamaanisha kuwa Sir Richard atakuwa amefanikiwa kuingia kwenye utalii wa anga na kushindana na mpinzani wake bilionea Jeff Bezos.
Muasisi wa biashara ya mtandao ya Amazon.com ambaye amewekeza fedha nyingi kujenga roketi na ametangaza safari yake kuwa Julai 20.
Aliwaalika watu watatu kuungana naye katika safari ya anga ambayo watatumia chombo chake kipya: kaka yake Mark; mtu ambaye hakutaka kufahamika aliyelipa dola milioni 28 (£20m) katika mnada wa kupata kiti na rubani wa kike maarufu Wally Funk.
Funk mwenye umri wa miaka 82, amepata mafunzo ya kuwa rubani wa anga mwaka 1960 na atakuwa mwendesha chombo cha anga mwenye umri wa juu Zaidi atakapoendesha roketi kwa umbali wa kilomita 100 akiwa na bwana Bezos.
Mmiliki wa Amazon hajatoa ufafanuzi wa namna tiketi zitakavyouzwa kwa ajili ya chombo chake kipya cha anga, lakini hii ni mipango yake.
Sir Richard amezindua safari yake ya kwanza ya anga katika kumjibu bwana Bezo ambaye alitaja tarehe ya mpango wa safari yake.
Ratiba ya safari ijayo ya ndege ya Unity itawataka wafanyakazi wanne wa Virgin Galactic kupanda kama abiria ili kufanya jaribio la chombo hicho kwa watalii watakaokuja siku zijazo.
Mara tu Sir Richard atakapopanda ndege na kufunga mkanda.Atakuwa miongoni mwa watu wanne ambao watafanya jaribio - akiwemo Beth Moses, mkuu wa muongozo wa Galactic katika kuongoza safari za anga; Colin Bennett, anaongoza operesheni za uhandisi; na Sirisha Bandla, makamu wa rais wa masuala ya serikali.
Rubani wawili mbele watakuwa Dave Mackay na Michael "Sooch" Masucci.
Utalii wa anga ni sekta ambayo imefanyiwa utafiti kwa muda mrefu.
Miaka ya 2000, matajiri saba walilipa kutembelea kituo cha kimataifa cha anga - International Space Station (ISS). Lakini safari hiyo iliandaliwa na Shirika la anga la Urusi ,na waliacha mpango wenyewe mwaka 2009.
Na sasa jitihada mpya zinakuja zikiwa zinalenga kuwa na maboresho ya juu Zaidi ya ndege za Sir Richard na Jeff Bezos.
Mjasiriamali wa teknolojia kutoka California Elon Musk tayari ameweka mipango ya kufanya misheni kadhaa za safari kutumia vyombo vyake vya Dragon capsules. Chombo chake kina uwezo wa kuruka Zaidi ya kilomita mia moja juu ya dunia na kukaa huko kwa siku kadhaa.
Warusi pia wanaandaa safari za anga za kibiashara kwa ISS, na wapo hata wale ambao wanataka kuanzisha vituo binafsi vya anga kwa ajili ya watu kwenda kutembelea.Miongoni mwao ni Axiom, kampuni ambayo ilianzishwa na meneja wa zamani wa mipango ya Nasa ISS.