Sherman: Hali ya chakula Korea Kaskazini ni ya kusikitisha
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Wendy Sherman leo amesikitishwa na hali ngumu na uhaba wa chakula wanaopitia raia wa Korea Kaskazini, mambo yanayohusishwa na janga la virusi vya corona. Hii ni baada ya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un hivi majuzi kuzungumzia hali mbaya ya chakula nchini humo na kukiri kwamba nchi yake inakabiliwa na mzozo mbaya zaidi kuwahi kuhushuhudiwa. Vilevile Sherman kwa mara nyengine ametoa wito wa kuitaka nchi hiyo kurudi tena katika mazungumzo ya mpango wa nyuklia. "Tunatazamia kupata maelewano na Korea Kaskazini. Kama alivyosema waziri wa kwanza wa mambo ya nje, tumejitolea kuketi chini na kuzungumza na Wakorea Kaskazini na tunasubiri kusikia kutoka kwao."Serikali ya Korea Kaskazini lakini imesisitiza kwamba haitorudi katika mazungumzo hayo ya nyuklia hadi pale Marekani itakapoacha ukatili wake. Mazungumzo kati ya nchi hizo mbili hayajapiga hatua tangu mapema mwaka 2019 pale mkutano wa pili wa kilele kati ya rais wa Marekani wakati huo Donald Trump na Kim Jong Un ulipokwama kutokana na mzozo wa vikwazo vya kiuchumi vilivyoongozwa na Marekani.