Wake wa Marais: Mfahamu Janet Kainembabazi Kataaha Museveni, mwanamke anayeaminiwa kuwa na ushawishi mkubwa Uganda

Museveni Bi Janet Kainembabazi Kataaha Museveni ni mmoja wa wake wa marais waliohudumu kwa muda mreefu

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI

Maelezo ya picha,

Bi Janet Kainembabazi Kataaha Museveni ni mmoja wa wake wa marais waliohudumu kwa muda mreefu

Ni watu wenye ushawishi katika uongozi wa kila siku wa nchi zao, hata hivyo si kila siku utasikia juu ya maisha yao na vipawa vyao. Hawa ni wenza wa marais, ambao baadhi yao ni wanasiasa na wanaharakati ambao wamekuwa bega kwa bega katika safari za kisiasa za wenza wao mpaka kushika hatamu za madaraka. Wiki hii tunakuletea mfululizo wa makala kuhusu wenza wa marais katika eneo la Afrika Mashariki na leo tunakupakulia yote unayofaa kujua kumhusu mke wa rais wa Uganda .

Mke wa Rais Museveni Bi Janet Kainembabazi Kataaha Museveni ni mmoja wa wake wa marais waliohudumu kwa muda mrefu katika wadhifa huo nchini Uganda, kutokana na mume wake Yoweri Kaguta Museveni kuwa mamlakani kwa muhula wa sita sasa. Sawa na wake wa marais wa Rwanda na Burundi Janet Museveni alionja maisha ya kuwa mkimbizi kabla ya kuwa mke wa rais.

Lakini je Maisha yake kabla ya kuwa mke wa rais yalikuwa vipi?

Bi Janet Museveni alizaliwa katika kaunti ya Kajara, wilayani Ntungamo, wazazi wake wakiitwa Bw Edward Birori na Bi Mutesi. Alipata elimu yake ya msingi katika shule msingi ya Kyamate na akaendelea na masomo ya sekondari katika shule ya wasichana ya Bweranyangi Girls' Senior Secondary nchini Uganda.

Alikimbia ghasia kufuatia mapiganao ya mwaka 1971, wakati Idi Amin alipoupindua utawala wa Milton Obote na wakati alipokuwa ukimbizini alikutana na Bw Yoweri Museveni na wakaoana.

Maisha na Bw Yoweri Museveni, watoto

Picha za maisha ya Bi Janet Kainembabazi Rutaaha na Bw Museveni kabla hajawa mke wa rais

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI /TWITTER

Maelezo ya picha,

Picha za maisha ya Bi Janet Kainembabazi Rutaaha na Bw Museveni kabla hajawa Mke wa rais

Bi Janet Kainembabazi Kataaha aliolewa na Yoweri Museveni mwaka 1973 na wakati utawala wa Idi Amin ulipoangushwa mwezi April 1979, alirejea nyumbani nchini Uganda kutoka Tanzania ambako alikuwa akiishi kama mkimbizi na mume wake.

Mwezi Februari 1981 wakati Yoweri Museveni alipoanzisha vita vya msituni dhidi ya serikali ya Obote, Janet Museveni na watoto wake walihama mjini Nairobi, Kenya ambako waliishi na marafiki wa familia hadi mwaka 1983.

Mwaka 1983, walihamia Gothenburg, Sweden, na kuishi huko mpaka mwezi Mei 1986, miezi minne baada ya jeshi la Yoweri Museveni la National Resistance Army kuchukua mamlaka mjini Kampala.

Bi Janet Museveni na Rais Museveni wakiwa na watoto wao watatu wa kike

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI/TWITTER

Maelezo ya picha,

Bi Janet Museveni na Rais Museveni wakiwa na watoto wao watatu wa kike

Muhoozi Kainerugaba

CHANZO CHA PICHA,MUHOOZI KAINERUGABA

Maelezo ya picha,

Mtoto wa kiume wa Bi Janeti Museveni na Bw Museveni - Jenerali Muhoozi Kainerugaba

Janet Kataaha Museveni na Rais Yoweri Museveni wamejaliwa watoto wanne, wa kiume mmoja na wa kike watatu, wa kwanza akiwa ni Muhoozi Kainerugaba ambaye alizaliwa 1974, Natasha Karugire aliyezaliwa mwaka 1976, Patience Rwabwogo aliyezaliwa mwaka 1978 na kitinda mimba akiwa ni Diana Kamuntu ambaye alizaliwa mwaka 1980.

Janet Museveni kama mke wa rais

Mara baada ya kurejea nchini Uganda kutoka ukimbizini , Bi Janet Museveni alianza harakati za uongozi kwa kuanzisha kile alichoita Juhudi ya Wanawake wa Uganda ya kuwaokoa yatima - (UWESO), shirika la kibinafsi alilolianzisha mwaka 1986, ambalo alisema alilianzisha kutokana na uzoefu wake kama mkimbizi.

Shirika hilo limekuwa likiwasaidia watoto mayatima kielimu ili kuboresha maisha yao na kuafikia malengo yao maishani.

Baadhi ya ya watoto yatima wa Uganda wanadaiwa kupata msaada wa kielimu kupitia shirika la UWESO lililoanzishwa na Bi Janet Museveni

CHANZO CHA PICHA,UWESO

Maelezo ya picha,

Baadhi ya ya watoto yatima wa Uganda wanadaiwa kupata msaada wa kielimu kupitia shirika la UWESO lililoanzishwa na Bi Janet Museveni

Kupitia shirika hilo pia akina mama kutoka maeneo mbali mbali ya Uganda wameweza kuhamasishwa kujiunga na vyama vya ushirika na kuweza kupewa mikopo midogo midogo ya kuendeleza shughuli zao. Baadhi yao kupitia wavuti wa UWESO wanatoa ushahidi wa mafanikio waliyoyapata kutokana na msaada wa UWESO.

Hali kadhalika Bi Janet Museveni alihusika sana katika kampeni za mapambano dhidi ya HIV na Ukimwi nchini Uganda katika miaka ya 1990, ambapo alibuni ushirikiano na mchungaji mwenye itikadi kali Martin Ssempa kutoa elimu ya kutoshiriki ngono nchini Uganda kama njia ya kuepuka maambukizi ya maradhi hayo.

Pia ni muasisi wa Mpango wa taifa wa maendeleo ya wanawake wa vijijini (NSARWU), Shirika lisilo la kiserikali -NGO linalowasaidia wanawake kwa kuwapatia uwezo wa kiuchumi.

Ni muasisi na mlezi wa Jukwa la vijana la Uganda- Uganda Youth Forum (UYF) shirika lisilo la kiserikali- linalozungumza na vijana kwa lengo la kubadili kujenga tabia na maadili ya kuwasaidia kujikinga na virusi HIV na Ukimwi.

Siasa na uongozi ulioibuautata

Bi Janet Museveni alianza kuonesha kiu ya kuingia katika siasa na uongozi wa juu nchini Uganda.

Mwezi Novemba 2005, alitangaza rasmi nia yake ya kugombea kiti cha ubunge katika Kaunti ya Ruhaama kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi wa Februari 2006. Aligombea kiti hicho dhidi ya mgombea wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC), Augustine Ruzindana, na kushinda kwa wingi wa kura. Alichaguliwa tena kwa muhula mwingine wa miaka mitano katika uchaguzi wa Machi 2011.

Kuteuliwa kwa Bi Janet Museveni kuwa na Raisi Yoweri Museveni Waziri kuliibua hisia kali miongoni mwa raia wa Uganda

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI/TWITTER

Maelezo ya picha,

Kuteuliwa kwa Bi Janet Museveni kuwa na Raisi Yoweri Museveni Waziri kuliibua hisia kali miongoni mwa baadhi ya raia wa Uganda

Kugombea ubunge kwa Janet Museveni kuliwashangaza raia Uganda, kutokana na kwamba lilikuwa jambo geni kwa Mke wa rais kugombea nafasi ya uongozi wa kisiasa kando na kuwa mke wa rais.

16 Februari 2009, Janet Museveni aliteuliwa na mume wake Rais Museveni kama Waziri mdogo anayehusika na masuala ya Karamoja na tarehe 27 Mei 2011, alipandishwa cheo na kuwa Waziri kamili wa masuala ya Karamoja.

Akiwa waziri wa masuala ya Karamoja alisifiwa kwa kuinua kiwango cha elimu miongoni mwa watu wa jamii ya Karamajong ambao ni wafugaji wa kuhama hama.

Tarehe 6 Juni 2016, baada ya mume wake kuchaguliwa tena kuwa rais , alimteua kuwa waziri wa elimu na michezo.

Kuteuliwa kwake kuwa waziri wa elimu na michezo, kulikosolewa vikali na baadhi ya ya Waganda hususan wasomi, ambao walihoji uwezo wake wa kielemu kuongoza wizara kubwa kama ya elimu, huku kukiwa na madai kuwa hakukidhi vigezo vya kujiunga na elimu ya chuo Kikuu, madai ambayo baadhi ya wasomi wanatofautiana nayo.

Baadhi ya maprofesa na wahadhiri wa Chuo Kikuu walidai kuwa hakuhudhuria masomo mara kwa mara, isipokuwa mara chache ambapo walimu walimfundishia Ikulu.

Licha ya madai hayo Bi Janet Museveni alitunukiwa shahada ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Makere nchini Uganda.

Licha ya Rais Museveni kukoselewa kwa kumteua mke wake kama Waziri, Bi Janet Museveni , ameendelea kuwa na wadhifa huo hadi leo.

Ushawishi

Janet Kainembabazi Kataaha Museveni anaaminiwa kuwa mmoja wa wake wa marais wenye ushawishi mkubwa kwa nchi zao barani Afrika, kutokana na nafasi za uongozi wa kisiasa kama vile ubunge na uwaziri sambamba na kuwa mke wa rais, kulingana na chambuzi mbali mbali kuhusu mamlaka na ushawishi walionao wake wa marais wa Afrika.

Bi Janet Museveni ni Waziri wa Elimu wa Uganda

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI /TWITTER

Maelezo ya picha,

Bi Janet Museveni ni Waziri wa Elimu wa Uganda

Baadhi ya wachambuzi wa ndani na nje ya Uganda wanaamini kuwa amekuwa na mchango mkubwa nyuma ya sera za serikali ya Uganda na baadhi ya maamuzi yanayochukuliwa na mume wake Rais Yoweri Museveni kuihusu nchi. Hata hivyo hakuna ushahidi unaothibitisha madai hayo.

Mtetezi wa mume wake

Anafahamika kwa kuwa mwanamke asiyetafuna maneno hasa anapomtetea mume wake dhidi ya wakosoaji wake na utawala wake na wale wanaodai kuwa wamechoshwa na utawala wake wa muda mrefu, na mara nyingine akitumia aya na mifano ya Biblia.

Wakati mmoja alisema mume wake ataendelea kuongoza :''kuwepo kwa muda mrefu madarakani kwa Rais Museveni pamoja na chama chake NRM ni utashi wa Mungu sio uchaguzi na rais atabakia mamlakani kwasababu bado anamuamini Mungu'', alinukuliwa na gazeti la The East African.

Alisema,''Wakati Mungu ana sababu ya mtu kuongoza nchi, ataendelea kumuweka katika nafasi hiyo hata kama watu wanataka vinginevyo, ili mradi ni chaguo lake''

Unapotizama ukurasa wake rasmi wa Twitter, utabaini kuwa jumbe zake nyingi zimehusishwa na Mungu au maandiko ya Biblia:

Ruka Twitter ujumbe, 1

Mwisho wa Twitter ujumbe, 1

Ruka Twitter ujumbe, 2

Mwisho wa Twitter ujumbe, 2

Haiba na muonekano

Sawa na wake wa marais wengine wa Afrika Mashariki , Bi Janet Museveni anaitwa ''Maama'', jina linalomaanisha mama na baadhi ya raia wa Uganda wanaomuenzi.

Mbali na siasa Bi Janet ana haiba na muonekano wa upole, hotuba zake zikitolewa kwa sauti tulivu, lakini yenye kufikisha ujumbe mzito kwa walengwa.

Ni Mkristo ambaye hotuba zake mara nyingi huambatana na mifano na aya za biblia kufikisha ujumbe kwa anaowalenga, lakini baadhi wanauona mtindo wa kutumia maandiko ya biblia kama njia yake ya kuwarai watu kuafiki anachokisema.

Ni Mkristo ambaye hotuba zake mara nyingi huambatana na mifano na aya za biblia kufikisha ujumbe kwa walengwa

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI/TWITTER

Maelezo ya picha,

Mtindo wa nywele zake asilia fupi ''Janet Cut'' umetokea kupendwa wanawake wa Uganda na nje ya mipaka yake

Mtindo wa nywele zake asilia zilizokatwa na kuwa fupi kichwani umetokea kupendwa na baadhi ya wanawake ndani na nje ya Uganda, pamoja na uso wake usiopakwa vipodozi, wakati mmoja mtindo wake wa ukataji nywele ulivuma na kupendwa huku baadhi wakiuita mtindo wake ''Janet Cut'', na kukata nywele zao kwa mtindo huo.

Mavazi yake yamekuwa ya aina mbili rasmi, suti za sketi ndefu au magauni marefu pamoja na vazi la kitamaduni linalovaliwa na mwanamke wa kabila lake la Banyankole.

Janet Museveni

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI/TWITTER

Janet Museveni, akiwa amevalia vazi la kitamaduni la kabila lake la Banyankole, alipokuwa akihuduria ibada mjini Kampala

CHANZO CHA PICHA,JANET MUSEVENI/TWITTER

Maelezo ya picha,

Janet Museveni, akiwa amevalia vazi la kitamaduni la kabila lake la Banyankole, alipokuwa akihuduria ibada kanisani mjini Kampala

Kutokana na kwamba Rais Yoweri Museveni ameendelea kuwa rais wa Uganda kwa muhula wa sita, na Bi Janet bado ni waziri wa elimu, ushawishi wa ''Maama'' ndani na nje ya Uganda hautarajiwi kuisha hivi karibuni.

Post a Comment

Please Select Embedded Mode To Show The Comment System.*

Previous Post Next Post