Saida Ahmed Rashid ni mwanamke wa aina yake , aghalabu kutokana na kuwa amejitokeza kimasomaso kuzungumzia maisha ya ndoa yake ya kwanza , ya pili , na sasa ya tatu ambayo anasema kuwa inaonekana kuendelea vyema kinyume na jinsi hali ilivyokuwa hapo awali katika ndoa zake za nyuma.
Bi. Saida anasema kujitokeza kwake kuzungumzia maisha yake na kuhusiana na maswala ya mahusiano kumeibua hisia tofauti.
Kuna wale ambao wanaosema kuwa mwanamke kutoka jamii yake ya Somalia hafai kujianika na kuzungumzia udhaifu wa ndoa , hata hivyo kuna wale ambao wamempongeza kwa kuwa kipaza sauti za shida na changamoto ambazo wanawake katika jamii yake wanapitia.
"Nilianza maisha ya ndoa wakati bado ninasoma , sitaki kusema kuwa nililazimishwa kuingia katika ndoa mapema , bali katika hali ya ujana liliniteka. Nilikutana na kijana mmoja ambaye tulipendana sana . Wakati huo nilijikuta nikiingia kwenye ndoa nikiwa na miaka 20 wakati nilipokuwa kidato cha tatu, "anasema Saida
Mwanamke huyu mwenye miaka thelathini ni mama ya watoto watatu anasimulia safari ya ndoa tatu ambazo zimekuwa ni somo kwake .
Na ndoto yake kuu ni kuwa mwanga kwa wanawake na pia wanaume wenye kukaa kwenye ndoa ambazo zinawapa uchungu na kero kuliko furaha inayotokana na ndoa .
Ndoa ya kwanza
Saida anasema ndoa yake ya kwanza , ilikuwa ni penzi la kwanza kwake , kwa hiyo ilikuwa na raha ya aina yake.
Aliingia kwenye ndoa hiyo mwaka 2008 , na kujaliwa mtoto mmoja wa kike ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 10 .
Changamoto kuu katika ndoa hii ilikuwa ni hali yao ya maisha . Katika hali ya kukithi mahitaji ya kila siku, kulikuwa na mahangaiko makubwa kati yake na mume wake wa kwanza .
Saida anasema hali ile iliwapelekea yeye ni mume wake kukubaliana kwa pamoja watafute njia ya kuondoka nchini Kenya. Mwaka 2010, Saida alisafiri hadi nje ya nchi kutafuta maisha .
"Mimi sikuwa na tamaa kubwa ya kutenganishwa na mume wangu , ila mume wangu alisisitiza kuwa aende ili kutafuta fursa za kuendeleza jamii yetu , kwa sababu ya siku za usoni , nisijue kuwa mahusiano yetu yangeanza kuporomoka kwa kuwa tulikuwa tumetenganishwa kimwili" , Saida anasema
Ndoa ilizidi kutokota mwaka huo alivyosafiri , na ikawa njia pekee ya kudumisha ndoa ilikuwa kupitia mitandao ya kijamii . Bila shaka wakati wa mawasiliano ya mbali mwanamke huyu anasema kuwa kulikuwa na shida ya saa maalumu ya kuwasiliana kutokana na mabadiliko ya saa kutoka bara la Afrika na bara Ulaya alipokuwa wakati huo
Ilipofikia mwaka wa 2013 ilikuwa dhahiri kuwa ndoa ilikuwa haina nguvu na ari ya kuendelea . Mwanadada huyu anasema kuwa mume wake pamoja na yeye walikubaliana kwamba ni wakati kila mtu aanze maisha yake upya .
"Ilikuwa sio jambo rahisi kukubali talaka , kwani wakati ninaondoka nyumbani kutafuta maisha nje ya nchi ya Kenya tayari nilikua nimemjulisha mume wangu nina shaka kuhusu ndoa yetu kutenganishwa , ila yeye ndiye aliyesisitiza kuwa tutafute maisha mazuri . Na hatua ya kwanza ilikuwa mimi kusafiri nje ya nchi .Kwa hiyo tulitengana kwa amani "anasema Saida.
Saida na mume wake walikubaliana jinsi ya kushirikiana kama wazazi wenza . Hadi sasa yeye na mume wa kwanza wanashirikiana katika malezi binti yao ambaye kwa sasa ana miaka kumi.
Kati ya mwaka 2012-2013 alipopewa talaka , hadi mwaka 2015, Saida alipiga moyo konde asiamini kuwa alikuwa mwanamke huru .
Kipindi hicho akilini mwake alikuwa anahoji ikiwa ni vyema aolewe tena au la .
Ndoa ya pili
Hatimaye mwaka wa 2015 alikutana na mwanamume ambaye walianza uchumba na baada ya muda waliamua kufunga ndoa.
Saida anasema kuwa mwaka wa kwanza hali ya ndoa ilinawiri na kama , ndoa nyingine mpya mapenzi yalinoga .Saida anasema kuwa mambo yalianza kuonekana kubadilika wakati aliposhika ujauzito wa tatu .
"Kipindi nilipoingia kwenye ndoa ya pili haikuchukua muda kwangu kushika mimba , nilipokea mtoto wa kiume ambaye tulimfurahia sana , wakati huyu mwanangu alihitimisha mwaka mmoja na miezi kadhaa nilishika mimba ya mtoto wa tatu , hili ni jambo ambalo sikulitarajia kwa hiyo nilikuwa kidogo na shaka na wasiwasi "anasema Saida.
Wakati wa ujauzito mahusiano yake na mume wa pili yalikuwa na doa , na ilikuwa wazi kwamba hawakuwa wanakubaliana katika maswala tofauti .
Saida alijaaliwa kujifungua mtoto wa kike ila licha ya hayo bado ndoa haikunawiri.
Mwanadada huyu anasema kuwa alihisi kana kwamba mume wake wa pili hakumuelewa vyema na mahitaji yake , kwa mfano anasema kuwa hawakuwa na muda wa kuketi kama wanandoa kwa kushirikiana kuleta ukaribu wao . Saida anahisi kutengwa na hapo ndipo alianza kuwa na msongo wa mawazo pamoja na sonona .
Hatua aliyoichukua mume wake ni kumpeleka hospitalini kumuona mwanasaikolojia , Saida anasema kuwa alikuwa ameshindwa kuzungumza na mume wake kuhusu shida za ndoa kwa kuwa alikuwa na uoga mwingi kutokana na kile anakitaja kama vita baridi ndani ya ndoa yake .
Saida anadai kuwa kadri siku zilivyokuwa zinasonga mume wa pili naye alianza hata kumdhulumu kwa kumchapa na pia kumdhulumu kisaikolojia .
Mwanadada huyu anasema kuwa alipoanza kuwa na mawazo ya kujitoa uhai , alijua kuwa mambo yalikuwa mabaya .
Vilevile saida anasema kuwa wakati wa patashika zake na aliyekuwa mume wake wa pili kisa kimoja kilichopelekea mwisho wa ndoa yake ni pale alitishia kumdunga kisu baada ya mzozo .
" Usiku wa mwisho wakati wa mizozo ya nyumbani , nilijikuta nimemtishia aliyekuwa mume wangu pili , kiasi cha kuwa alijifungia katika chumba chetu hadi asubuhi. Kesho yake wazee waliitwa , nami pia nilimjulisha baba yangu kuhusu kisa hicho . Iliamuliwa kuwa haikuwa na haja ya kuendelea kukaa katika ndoa iliyokuwa na dhuluma . Nilipewa talaka yangu ya pili baada ya hapo", anasema Saida.
Ndoa ya tatu .
Talaka ya pili ilifanyika mwaka wa 2017 , huku Saida akiapa kuwa hatajaribu kuingia kwenye ndoa wala uhusiano mwingine. Wakati ndoa ya pili inaporomoka watoto wake wawili aliojaliwa katika ndoa ya pili walisalia na baba yao. Pia kule kutenganshwa na watoto wake kulifanya maisha kuwa magumu kwa kuwaza jinsi ataishi bila kuwaona .
Katika pilkapila hizo Saida alianza mahusiano mengine ya kimapenzi na mambo yalikwenda haraka hadi akajikuta ameolewa mara ya tatu.
"Nilikuwa nimeapa kuwa sitaolewa tena , lakini unajua kuwa mimi ni binadamu , na kama kawaida ya binadamu tunahitaji kupendwa na kudekezwa hasa sisi wanawake , mapenzi niliyoyahisi kwa huyu mume wangu wa tatu yalizidi kero niliyokuwa nayo katika ndoa ya pili , kwa hivyo mimi nimeshapiga moyo konde na kuamua kuanza maisha upya "anasema Saida.
Saida anataraji kuwa , ndoa ya tatu itanawiri , anasema kuwa kufwatia shida na pandashuka za ndoa ya kwanza , kwa upande wake atahakikisha ametekeleza wajibu wake kama mwanamke . Vilevile anasema kuwa panapokuwa na nia nzuri mambo yote huenda sawa .
Saida anasema kuwa simulizi ya safari yake ya ndoa kunaibua gumzo hasa miongoni mwa baadhi ya watu wa jamii yake ya Wasomali , kwa kuwa mambo ya ndoa huwa hayazungumziwi hadharani . Akiwa yeye ni mwanamke inakuwa na changamoto zaidi, Kwani Saida anasema kuwa sio wanawake wengi huzungumzia changamoto katika ndoa .
"Ninapata maoni tofauti kuhusiana na hatua yangu ya kuzungumzia safari yangu ya ndoa , ninaamini kuwa simulizi yangu huenda ikawasaidia mabinti na pia vijana wengi wa kike , sio tu wa jamii yangu ila kwa ujumla wake . " Saida anasema.
Saida ni mmoja wa wale wenye kuamini kuwa dhuluma za kisaikolojia/ kiakili zina uwezo wa kusababisha magonjwa ya kiakili.
Na Kwa hiyo anapendekeza kuwa iwe. ni mwanaume au mwanamke ambaye anapitia haya , yakiendelea kwa muda huwa na athari mbaya katika hali ya kisaikolojia ya mtu .
Saida anapendekeza wanawake kutokaa kwenye ndoa zenye ukatili wa kichapo au dhulumu nyingine , Kwani mwisho wa siku wanawake kama yeye ambao wamepitia hali hii , bila suluhisho kupatikana ndani ya ndoa huwa na machungu na kero, ambazo zikiongezeka huenda zikawa hatari mno . Kwa mfano mienendo ya kulipiza kisasi, mawazo ya kujitoa uhai au kutenda maovu.