Na Dinah Gahamanyi
BBC Swahili
Ugonjwa wa Ebola si ugonjwa unaofahamika kuwa miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana, kama vile kaswende, kisonono na ukimwi na mengine, ambayo yamekuwepo kwa muda mrefu.
Hata hivyo baada ya ugonjwa huu kuenea katika mataifa ya Magharibi, Mashariki na kati mwa Afrika imegungulika kuwa ugonjwa huu unaoweza kuua kwa haraka unaweza kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana, hata baada ya mgonjwa kupona. Hii imewafanya wataalamu wa ugonjwa huo, wakiwemo watafiti na madaktari kuwashauri watu walioambukizwa na hata manusura wa Ebola waepuke tendo la kujamiiana siku 90 baada ya kupona.
Ebola ni nini?
Ni virusi hatari vyenye dalili za awali ambazo zinaweza kujumuisha homa ya ghafla, udhaifu mkubwa, maumivu ya misuli na koo.
Dalili zinazofuata zinaweza kujumuisha kutapika, kuhara na katika hali nyingine kutokwa na damu ndani na nje, inayojulikana kama haemorrhaging.
Je ni kwanini manusura wa Ebola wanashauriwa kuepuka tendo la kujamiiana kwa siku 90?
Ingawa ugonjwa wa Ebola haujakuwa ukichukuliwa kama maradhi yanayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana(ngono), katika baadhi ya tafiti, wataalamu wamebaini kuwa virusi vyake vinaweza kusambazwa kwa njia ya hiyo hata baada ya wagonjwa kupona.
Akizungumza na makala hii, Daktari Frank Bawela kutoka katika kituo cha tiba mjini Kampala Uganda- nchi ambayo inakumbwa na maambukizi ya Ebola, analinganisha virusi vya Ebola na HIV cha Ukimwi, kwa namna kinavyoambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine.
Huku idadi ya maambukizi ya Ebola ikiendelea kuongezeka kwa kasi nchini Uganda, binafsi Dkt Bawela anajiandaa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa Ebola, iwapo watafika kwenye kliniki yake. Jumla ya visa 43 vya maambukizi vimeripoliwa na wizara ya afya nchini Uganda huku tisa kati yao wakifariki.
Dkt Bawela anasema: ‘’ Virusi vya Ebola huishi ndani ya mbegu za uzazi za kiume, na maji maji au ute wa mwili, ikiwa ni pamoja na mate, sawa na HIV, na hivyo mgonjwa wa Ebola anaweza kusambaza virusi kwa mtu mwingine kwa njia hii’’, anasema Dkt Bawela.
Hoja yake haitofautiani na hoja za madaktari, watafiti na wataalam wengine waliofanya kazi zao kuhusu Ebola.
Dkt Ataro Ayella, daktari wa magonjwa yanayoambukiza, ambaye alihudumu katika milipuko ya awali ya Ebola katika Wilaya ya Bundibugyo mwaka 2007, Liberia mwaka 2014, na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika mwaka 2019, aliliambia gazeti la Monitor katika mahojiano tofauti alisema kwamba virusi vya Ebola vinaweza kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana na kuishi katika mbegu za kiume hadi kufikia miezi mitatu.
Hii inamaanisha kuwa maambukizi hayo yanaweza kutokea hata kama mtu aliyenusurika nae bola haonyeshi dalili zozote za ugonjwa.
Dkt Frank Bawela ameiambia BBC kuwa ni vyema mtu aliyeathirika na Ebola ajihadhari kujamiiana na mwenza wake hata baada ya situ 90.
‘’Ni vizuri kwa mfano kwa wanandoa kupima tena baada ya siku 90 kupatikana bila virusi, ili kuhakikisha kabisa kwamba vitusi vimeisha katika mwili wako’’, anasema.
''Na kwa wanandoa pale mnapoona ni lazima kujamiiana baada ya siku 90 kabla ya kupimwa basi watumie mipira ya kinga na kuhakikisha kuwa iko vyema, ili kuzia maambukizi’’, anasisitiza Dkt Bawela.
Wanasayansi wnasema tafiti zilizofanywa nchini Liberia zinaonyesha mwanamke aliyeathiriwa na Ebola kufuatia kufanya tendo la ngono na mwanaume aliyenusurika na ugonjwa huo kutoka nchi jirani.
“Licha ya kupona ugonjwa, maambukizi baina ya mtu aliyepona na mtu mwingine ambaye hana ugonjwa huo yanaweza kutokea ... Maambukizi hayo hutegemea uthabiti wa kinga ya mwili ya mtu na magonjwa mengine ambayo tayari anayo ,” anasema Dkt Ayella.
Alhamisi juma lililopita , akizungumzia kuhusu Ugonjwa wa Ebola ambao sasa umeikumba nchi yake na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 40, alisisitizia kuhusu kuepukwa kwa tendo la ngono baada ya kupota Ebola:
‘’Ebola husambazwa kwa kiwango cha juu zaidi kupitia mgusano na maji maji ya mwili. Njia nyingine ni iwapo utafanya ngono, mate na kuongezewa damu. Habari njema ni kwamba haiambukizi sawa na Covid-19 ambao ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya hewa’’ alisema Museveni’’
Mwisho wa Twitter ujumbe
Mkurugenzi katika wizara ya afya anayehusika na hutuma za tiba nchini Uganda , anasema Ebola virus hujificha katika mifuko ya mbegu za uzazi baada ya mgonjwa kupona.
Wataalamu mbali mbali wa Ebola wanasema virusi vinaweza kujificha katika maeneo mengine ya mwili kama vile maji maji ya uti wa mgongo na kwenye machozi ya macho.
Maradhi ya Ebola yanasambaa vipi?
Ebola imefika kwa binadamu kutoka kwa wanyama walioambukizwa, kama vile sokwe, popo na swala wa msituni.
Nyama ya msituni - wanyama wa porini wanaowindwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu inadhaniwa kuwa hifadhi ya asili ya virusi.
Kisha huenea kati ya binadamu kwa kugusana moja kwa moja na maji ya mwili wa mtu mwenye virusi kama vile damu, mate, matapishi, shahawa, uchafu ukeni, mkojo, kinyesi na jasho.
Wanaume ambao wamepona Ebola pia wamekutwa na virusi kwenye shahawa zao kwa muda baada ya kupona.
Ni tahadhari gani zaidi zinaweza kuchukuliwa kudhibiti ebola?
Ili kuzuia maambukizo, wataalamu wa afya wanashauri kuepuka kugusana na walioambukizwa, ikiwa ni pamoja na kuacha kupeana mikono, kunawa mikono kwa sabuni na maji na kusafisha nyuso kwa maji ya klorini.
Pia ni muhimu kutenganisha wagonjwa na watu wanaokutana nao walio kwenye mawasiliano.
Kwa kawaida nchi huweka vituo kwa ajili ya kesi zinazoshukiwa na vituo vya matibabu kwa kesi zilizothibitishwa kimaabara.